Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu (Mb.) amemuaga Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) Dk. Natalia Kanem anayetarajia kuondoka nchini hivi karibuni mara baada ya kumaliza muda wa uwakilishi wa shirika hilo hapa nchini.

Akizungumza na mwakilishi huyo Ofisini kwake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy ameeleza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sera, miongozo na sheria mbalimbali zinazohusu usawa wa jinsia na haki za watoto hususan watoto wa Kike.

Amesema Serikali itaendelea kufanya kazi na kushirikiana na UNFPA pamoja na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya Tanzania.

Ameleza kuwa wizara yake itaendelea kuhakikisha kuwa tatizo la ukatili dhidi ya watoto linalohusisha ndoa na mimba za utotoni, ubakaji na ulawiti kwa watoto linamalizika katika jamii ya watanzania

Aidha,amesema kuwa wizara yake itaendelea na juhudi za kupunguza vifo vya mama wajawazito kwa kuweka miundombinu na mazingira bora ya kujifungulia   huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuelimisha na kuhamasisha umma wa watanzania juu ya umuhimu wa kuzingatia uzazi wa mpango.

Kwa upande wake Dk. Natalia Kanem ambaye alikua  ameambatana na Mratibu Mkazi  wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa hapa nchini Tanzania, Alvaro Rodriguez ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano iliyompatia katika kipindi chote alichokuwa hapa nchini na kuahidi kuendeleza kudumisha mashirikiano hayo atakapokuwa Makao Makuu ya Shirika hilo

Serikali Yawataka Watendaji Kupanda Miti Hekta 185,000 Kwa Mwaka
Mtu Mmoja Akamatwa Nchini Nigeria Kwa Kumuita Mbwa Wake Jina La Rais Wa Nchi Hiyo