Vyeti kila mtu anavyo tena vyenye madaraja mazuri na ang’avu, katika kundi kubwa la waombaji kazi kitu pekee na cha tofauti kinachoweza kuonesha uwezo wa mtu juu ya nafasi aliyoomba ni uwezo mkubwa wa kushawishi katika barua yake ya maombi ya kazi.

Cha ajabu ni kwamba barua nyingi za kazi hutia waajiri wengi mashaka na wasiwasi mkubwa kabla hata hatua ya pili ya usaili kufika.

Nimebahatika kuwa na rafiki yangu wa karibu ambaye ni Meneja Rasilimali Watu (HR) wa taasisi moja kubwa hapa nchini, kwa ufupi ndiye kiungo muhimu cha ajira katika taasisi hiyo. Tulisoma darasa moja tulipokuwa shule ya msingi!.

Kilio kikuu kama changamoto yake ni simu anazopigiwa na watu anaofahamiana nao wakimuomba awasaidie kupata ajira kwenye taasisi hiyo, “fanyafanya basi tuingie hapo.” Kwa bahati nzuri, ajira zinapotangazwa huwatafuta wote anaowafahamu na kuwapa tangazo hilo ili waombe kama watu wengine, waingie kwenye usaili. Cha ajabu, anasema ingawa wengi huwa na sifa na vyeti vyenye alama ng’aavu, barua zao za kazi humuacha hoi na kumpa wasiwasi muajiri hata kabla ya usaili wa hatua ya pili.

Nimesema usaili wa hatua ya pili! ndiyo, kwani usaili wa kwanza na muhimu zaidi huwa ni ule wa kupitia nyaraka zilizowasilishwa na waombaji. Barua ya kazi ikiwa na umuhimu wa kwanza, kisha Wasifu (‘Curriculum Vitae’) na baadaye kuhakiki vyeti husika.

Rafiki yangu Meneja Rasirimali watu aliniambia kuwa kama kazi inakuwa na waombaji wengi, zoezi la kwanza sio kuwatafuta wenye sifa, bali ni kuwatafuta wasio na sifa, waliokosea vigezo na wasioeleweka (Elimination Method).

Ingawa wengi huichukulia poa barua ya kazi, ukweli ni kwamba makampuni yaliyo makini huichambua vizuri barua yako ya kazi kabla ya kugusa CV na mwisho kukagua vyeti. Na hii ndiyo sababu baadhi ya makampuni huomba barua iliyoandikwa kwa mkono. Ubovu wa barua ya kazi ni sehemu ya chanzo cha wengi kutoitwa kwenye usaili.

Ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani wamjibu Tundu Lissu
Video: Malima awasha moto sakata la Diwani kukunja nne kikaoni