Umoja wa Mataifa umetangaza msaada wa dharura wa Dola Milioni 35.6 kwa raia waliokumbwa na mapigano katika jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia.

Katika fedha hizo Dola Milioni 25 zitapelekwa Ethiopia ili kununua dawa na vifaa vya matibabu, ili kuwasaidia raia wanaougua au waliojeruhiwa, na kununua chakula na kuwapa maji ya kunywa. 

Katika nchi jirani Sudan, ambako watu 50,000 wamekimbilia tangu mapigano hayo yalipoanza, kiasi kingine cha dola milioni 10.6 kinapelekwa ili kuwasidia wakimbizi hao. 

Wakati huo huo, misafara ya magari yaliyobeba msaada wa kibinadamu yameanza kuwasili katika jimbo la Tigray, ambalo lilikuwa katika mapigano wakati wa vita baina ya vikosi vya serikali kuu na chama cha ukombozi wa watu wa Tigray TPLF, kinacholiongoza jimbo hilo. 

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema misafara hiyo ilipeleka maelfu ya tani za vyakula, na kuongeza kuwa bado hali sio ya kuridhisha.

Nigeria: Wanafunzi 344 waliotekwa waokolewa
Daraja la Busisi lapewa jina la Magufuli