Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema umoja huo hautounga mkono hatua ya kuiwekea tena Iran vikwazo, kama ambavyo Marekani inataka hadi hapo atakapopewa idhini na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Guterres amesema kuna hali ya sintofahamu iwapo waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo ameanzisha mchakato wa kurejesha vikwazo katika azimio la Baraza la Usalama ambalo lilitia saini makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na nchi sita zenye nguvu duniani au la.

Siku ya Jumamosi Serikali ya Marekani ilitangaza kuwa vikwazo vyote vya umoja wa mataifa dhidi ya Iran vimerejeshwa, hatua ambayo imepingwa na mataifa mengine duniani yakisema havina uhalali na vinafaa kupuuzwa.

Wachambuzi wanasema tangazo hilo la Marekani huenda litasababisha utata wakati wa mkutano wa maafisa wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoanza leo, ambao unafanyika kwa njia ya video kwa sababu ya janga la COVID-19.

Guterres amesema Baraza la Usalama la umoja wa mataifa halijachukua hatua yoyote baada ya kupokea barua ya Pompeo, wala hakuna mwanachama wake yeyote au rais ambaye amechukua hatua.

Shule kufunguliwa Oktoba - Kenya
DPP aagiza uchunguzi fedha za Covid 19 - Kenya