Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameelezea masikitiko yake kufuatia shambulio la leo la kombora dhidi ya mji wa Vinnytsia ulioko eneo la kati nchini Ukraine, shambulio lililosababisha vifo vya takribani watu 22. 

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric inasema Katibu Mkuu analaani shambulio hilo ambalo miongoni mwa waliouawa ni watoto watatu huku zaidi ya watu 100 wamejeruhiwa.

Vyombo vya habari, vinaripoti kuwa shambulio hilo la kombora limefanyika majira ya asubuhi kati kwa kwa saa za Ukraine wakati mitaa ya mji huo ikiwa na watu wengi.

Guterres, amerejea wito wake kwa pande kinzani kwenye mzozo huo kuzingatia sheria za kibinadamu za kimataifa kwa kuhakikisha kuwa maeneo ya kiraia pamoja na raia hayashambuliwi.

“Katibu Mkuu ametaka pia wahusika wa shambulio hilo wawajibishwe kisheria,” imesema taarifa hiyo.

Shambulio hilo, limefanyika siku moja tu baada ya mkutano huo uliofanyika kwenye makao makuu ya Mahakama ya Kimataifa ya makosa ya jinai, ICC ya The Hague Uholanzi kujadili uwajibikaji wa makosa ya uhalifu wa kivita nchini Ukraine.

ICC inasema, mkutano huo ni muhimu katika jitihada za pamoja za kusaka haki kwa madai ya uhalifu wa kivita nchini humo.

Masharti ujenzi vituo vya mafuta yalegezwa
Mongella aagiza usimamiaji miradi kwa weledi