Umoja wa Mataifa umempongeza Rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, baada ya kula kiapo cha kuiongoza nchi hiyo na kuahidi kuipa ushirikiano kwa serikali yake katika kutimiza vipaumbele vya nchi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amesema wanamuhakikishia Rais huyo ushirikiano, na kwamba wana imani atatekeleza yale yote ambayo ni mapungufu katika nchi hiyo.

“Pongezi kwa Rais Mohamud na UN inakuhakikishia ushirikiano katika kutimiza vipaumbele ulivyojiwekea kwenye uongozi wako ili kuwatumikia wana Somalia,” alisema Guterres.

Sherehe za kuapishwa kwa Rais huyo wa kumi zilifanyika katika eneo la Hangar lililopo uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Aden Adde Juni 9, 2022 na kuhudhuriwa na wawakilishi mbalimbali wa kitaifa, kimataifa, wakuu wa nchi na Wananchi wa Somalia.

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, Adam Abdelmoula, Naibu Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa ni kati ya Viongozi wa kimataifa waliohudhuria sherehe za uapisho huo.

Wengine ni Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh na Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu kutoka UN wa nchini Somalia. 

Katika sherehe hizo pia alikuwepo Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Taban Deng Gai na Waziri Mkuu wa Misri Mostafa Kamal Madbouly. 

Nchi nyingine zilizowakilishwa katika sherehe hizo za uapisho ni Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Uganda, Burundi na Turkiye. 

Balozi Mulamula awasilisha Ujumbe Maalum wa Rais Samia kwa Rais wa Misri
Makamba: Serikali haijapandisha bei ya umeme