Umoja wa Mataifa (UN), umesikikitishwa na vifo vya waafrika 23 na wengine zaidi ya 76 kujeruhiwa wakati wakijaribu kuvuka mpaka katika ya Morocco na Hispania ili kwenda barani Ulaya kupitia mpaka wa Mellila na Ceuta.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Ravina Shamdasani akiwa mjini Geneva Uswisi imesema tukio hilo lililotokea Juni, 24 2022, linapaswa kuchunguzwa kwa umakini na uhuru kwa nchi zote mbili ili waliohusika na kusababisha vifo na majeruhi hao wachukuliwe hatua za kisheria pamoja na kuwajibishwa.

Shamdasani amewaambia waandishi wa Habari kuwa, hiyo ni idadi kubwa zaidi ya vifo vya wahamiaji kurekodiwa katika tukio moja baada ya miaka mingi na kudai kuwa Ofisi ya haki za kibinadamu ilipokwa ripoti za wahamiaji hao wanaodaiwa kuchapwa fimbo, kupigwa mateke, kushambuliwa kwa mawe na kutupwa ardhini.

Amesema, kitendo hicho kilifanywa na maafisa wa usalama wa Morocco, kufuatia waafrika hao kujaribu kuinua waya wenye unatenganisha Morocco na Melilla na
katika harakati hizo za kuwazuia kuvuka mpaka askari wa Morocco wapatao 140 wameripotiwa kupata majeraha.

“Tunatoa wito kwa Morocco na Hispania kuhakikisha wanaheshimu haki za binadamu za wahamiaji katika mpaka wao wa pamoja na maafisa walio mpakani waepuke matumizi yoyote ya nguvu kupita kiasi dhidi ya wahamiaji,” Amesema Shamdasani.

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa, pia imetaka kuchukuliwa kwa hatua za haraka kupitia Jumuiya ya Ulaya, Umoja wa Afrika na wahusika wengine wa Kimataifa na Kikanda, ili kuhakikisha kunakuwepo na utawala bora unaozingatia haki za binadamu mipakani.

“Hatua hizo ni pamoja na kuhakikisha kuna njia salama za wahamiaji kupita, kufanyika kwa tathmini binafsi za kila mtu anayetaka kupita mpakani, pamoja na kuwahakikishia ulinzi dhidi ya kufukuzwa kwa pamoja au kukamatwa na kuwekwa vizuizini kuholela,” imesisitiza Ofisi ya UN.

Katika hatua nyingine, Ofisi ya Kamishna Mkuu imesema imesikitishwa na ripoti ya kupatikana kwa takriban miili ya watu 46 ndani ya lori huko San Antonio Texas nchini Marekani, ikihisiwa kuwa ni ya wahamiaji haramu waliokuwa wakivuka mpaka kutona nchini Mexico.

Hili si tukio la kwanza la aina hiyo kutokea huku likionesha uwepo wa umuhimu wa uchunguzi wa mara kwa mara wa njia salama kwa wahamiaji, pamoja na kuhakikisha uwajibikaji na kuwachukulia hatua wote wanaohusika na usafirishaji wa aina hiyo na kusababisha vifo vya watu.

Wakili atinga Mahakamani na vazi la ‘sangoma’ jaji aahirisha kesi

Wanahabari wajiuliza marekebisho vifungu vya sheria
Rekodi za vifo vya raia nchini Syria inatisha