Huko nchini Kenya katika eneo la Baricho, Kirinyaga imetokea vuta nikuvute baada ya wasichana kudai fedha zao kwa mchungaji waliyemlipa ili awaombee wapate wanaume wa wakuwaoa.

Wasichana hao wamelalamika kuwa, maombi ya mchungaji huyo anayejiita Nabii hayajafanya kazi licha ya kulipwa fedha kwani hata salamu kutoka kwa wanaume zimekata tofauti na awali kabla hawajaombewa.

Inadaiwa kuwa Nabii huyo ambaye ni Mwanamke awali alitambulika na wengi kutokana na maombi yake kwa warembo waliokuwa hawajafanikiwa kupata waume.

Kwa mujibu wa gazeti la Taifa Leo, wasichana wengi walikuwa wakifurika kwa mama huyo kusaka maombi ambayo walilazimika kuyalipia kabla ya kuhudumiwa.

Lakini awamu hii mambo yamekuwa kinyume kwani baada ya kufanyiwa maombi inasemekana wasichana hao waliahidiwa kusubiri kwa muda wa siku tatu kabla ya kuanza kuona matokeo.

Hata hivyo siku tatu zilipita, wiki nayo pia ikaisha bila warembo kuona mabadiliko yoyote na walipogundua walikuwa wameahidiwa waliamua kurejea kwa mama huyo.

“Tunataka hela zetu, ulituambia tutaanza na kupata wanaume wa kutuoa baada ya siku tatu. wako wapi? , juzi nilitongozwa hata saa mbili hazikupita jamaa akaniblock. Maombi yako ni ya laana ama Baraka,” alilalamika mrembo mmoja huku Nabii huyo akibaki mdomo wazi.

Hata hivyo baada ya kelele kuzidi mama aliwaomba awafanyie maombi mengine huku akidai kwamba huenda wasichana hao hawakuweka imani ya kutosha.

Manula, Bocco waivuruga Simba SC Harare
Ntibazonkia: Msimu huu tutakuwa mabingwa