Meneja wa klabu ya Arsenal Unai Emery amesema anaheshimu na kuthamini mawazo ya kiungo Mesut Ozil, baada ya kutangaza kujiuzulu kuitumikia timu ya taifa ya Ujerumani.

Ozil alitangaza kuachana na timu hiyo mwishoni mwa juma lililopita, baada ya kuchukizwa na tuhuma alizorushiwa na wadau wa soka nchini humo, kufuatia picha aliyopiga na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mwezi Mei jijini London, wakati wa maandalizi ya fainali za kombe la dunia.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29, anaamini jambo hilo ni sawa na ubaguzi wa rangi pamoja na kumkosea heshima yeye kama mchezaji, hivyo aliona bora ang’atuke kwenye kikosi cha Ujerumani.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari huko Singapore walipoweka kambi ya kuajiandaa na msimu mpya wa ligi, meneja wa Arsenal Emery amesema: “Sote tunapaswa kuheshimu maamuzi yake, tunapaswa kumuonyesha ushirikiano baada ya kutangaza maamuzi hayo, sioni sababu za jambo hili kuendelezwa katika vyombo vya habari wakati mchezaji ameshaamua.”

“Ni jambo binafsi na mimi ninaliunga mkono, tunachofanya hivi sasa ni kuendelea kufanya kazi na Ozil na tangu alipojiunga na kambi mwishoni mwa juma amekua mwenye furaha wala haonyeshi kama kuna jambo lilimkwaza siku za nyuma.”

Kuhusu mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Atheltico Madrid utakaochezwa kesho huko Singapore, meneja huyo kutoka nchini Hispania amesema kikosi chake kipo tayari baada ya kufanya mazoezi kwa siku kadhaa tangu walipowasili huko mshariki ya mbali.

Baada ya mchezo huo, Arsenal watapamba na mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris St Germain Julai 28.

Agusti Mosi Arsenal itacheza dhidi ya Chelsea mchezo wa kirafiki, kabla ya kurejea England, tayari kwa mchezo wa ufunguzi wa ligi dhidi ya Man city Agusti 11.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 26, 2018
TFF yabadilisha mfumo U20, yatambulisha U15, U17

Comments

comments