Hatimae mabingwa wa soka nchini Ufaransa, Paris Saint-Germain wememtangaza mrithi wa Laurent Blanc aliyeondoka siku chache zilizopita kwa kigezo cha kushindwa kufanya vyema kimataifa.

PSG, wamemtangaza aliyekua meneja wa klabu ya Sevilla, Unai Emery kuwa mkuu wa benchi la ufundi, kwa kuamini atafanikisha azma ya kufanya vyema na kutimiza lengo la kutwaa ubingwa wa barani Ulaya.

Emery, aliiongoza Sevilla kutwaa ubingwa wa Europa League mara tatu mfululizo, kabla ya kutangaza  kujiuzulu mapema mwezi huu.

Mbali na kuwa meneja, pia Emery aliwahi kuwa mchezaji wa klabu ya Real Sociedad katika nafasi ya kiungo na alianza shughuli za ukufunzi mwaka kuanzia 2008-12 akiwa na Valencia, na kisha alijiunga na Andalusia kabla ya kutimkia Sevilla.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari uliomtambulisha rasmi kama meneja mpya wa PSG,  Emery alisema imekua faraja kubwa sana kwake kujiunga na klabu hiyo, na anaamini kwa ushirikiano atakaoupata utamuwezesha kufikia malengo yanayokusudiwa.

“Ni faraja kwangu kuwa sehemu ya klabu hii kubwa na kongwe hapa Ufaransa, na ninaamini mambo yatakaa sawa kutokana na mazingira niliyokutana nayo hapa,

“Klabu hii imepata nafasi ya kuwa na umaarufu mkubwa miaka ya hivi karibuni kutokana na nguvu zilizowekezwa hapa, na ninaamini suala hilo litanifanikishia kazi yangu kuwa kwenye mustakabali mzuri,

“Nina hamu ya kuwa sehemu ya watakaoipa mafanikio klabu hii, na jambo hilo linawezekana kufuatia nguvu kubwa ya ushirikiano niliyoiona tangu nilipowasili jijini Paris.” Alisema Emery

Naye mwenyekiti na mmiliki wa klabu ya PSG, Nasser Al-Khelaifi alidhihirisha furaha yake mbele ya waandishi habari katika mkutano huo, kwa kusema ni hatua nzuri waliyofikia na wanakusudia makubwa zaidi baada ya kufungua ukurasa mpya wa kuwa na meneja atakaeleta chachu ya mafanikio.

“Tunaamini Unai ataleta utofauti mkubwa katika klabu hii, kutokana na uzoefu wake mkubwa alioupata akiwa na Sevilla ya nchini Hispania, nimefarijika sana kwa kufikia makubaliano na mtu huyu.” Alisema Nasser Al-Khelaifi

Unai Emery, huenda kaanza shughuli zake kwa kutaka kufanikisha mengi mazuri klabuni hapo, kutokana na meneja aliyemtanguliwa Laurent Blanc kutwaa mataji 11 ya michuano ya nchini Ufaransa, ndani ya miaka mitatu ya ajira yake.

England Kuachana Na Makocha Wazawa
Mabomu ya Kigaidi yaua makumi uwanja wa ndege Uturuki