Kipande cha video kilichotua mtandaoni kikimuonesha mwanamke mjane raia wa Kenya akiwapikia mawe wanaye wanane kwa lengo la kuwadanganya kuwa anawapikia chakula ili walale na kuvusha usiku, kimebadili maisha ya mwanamke huyo baada ya kupokea mamilioni ya fedha kutoka kwa ‘Wasamalia wema’.

Peninah Bahati Kitsao, mwanamke mjande anayeishi Mombasa nchini Kenya alirekodiwa na jirani yake, Prisca Momanyi katika harakati za kuwadanganya watoto wake baada ya kukosa chakula cha kuwapikia. Aligusa mioyo ya watu wengi hasa baada ya kuhojiwa na kituo cha runinga cha NTV.

Bi. Manyoni ndiye aliyekifikisha kipande cha video hiyo mtandaoni na kuvifikishia taarifa vyombo vya habari ili kujionea uhalisia wa ugumu wa maisha uliokuwa unamkabili jirani yake.

Katika mahojiano aliyofanya na NTV, Bi. Kitsao mwenye watoto nane, asiyejua kusoma na kuandika, alieleza kuwa alikuwa anafanya kazi za kuwafulia nguo watu majumbani kwao, lakini hivi sasa hali imekuwa ngumu baada ya mwingiliano wa watu kuzuiwa kutokana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Mwanamke huyo mwenye watoto nane anaishi kwenye nyumba duni yenye vitanda viwili vya kulala. Mume wake alipoteza maisha mwaka jana baada ya kuvamiwa na majambazi waliomuua kwa vipigo.

Kupitia mahojiano hayo, alisema kuwa wanae nane walibaini kuwa alikuwa anawadanganya kwa kwakuwa alipika kwa muda mrefu ‘mawe yake’, lakini hakuwa na jinsi.

“Wanangu walianza kuniambia kuwa wanajua nawadanganya, lakini sikuwa na jinsi kwakuwa sikuwa na kitu chochote,” Bi. Kitsao alisimulia.

Jirani yake alilazimika kufika kwenye nyumba hiyo baada ya kusikia watoto wakilia sana usiku huo. Ndipo alipokutana na mbinu ya ‘kupika mawe’ iliyomuumiza moyo.

Baada ya habari yake kuwa maarufu mitandaoni, jirani yake alipewa mamlaka ya kukusanya michango kupitia akaunti ya benki na simu benki; ndipo makampuni na taasisi yalipomuunga mkono ikiwa ni pamoja na ‘Shirika la Msalaba Mwekundu’.

Serikali ya Kenya imeandaa mpango wa kugawa vyakula kwa watu wasiojiweza katika maeneo ambayo watu wamezuiliwa majumbani kwao (lockdown). Kwa habati mbaya mpango huo ulikuwa bado haujapiga hodi kwa Bi. Kitsao. Hadi sasa nchi hiyo ina visa 395 vya corona na vifo 27 vilivyotokana na ugonjwa huo.

Umoja wa Mataifa, Marekani wazungumzia alipo Kim Jong-un

Waziri Mkuu wa Urusi aambukizwa corona, awekwa karantini

TANZIA: Waziri Mahiga afariki dunia, Rais Magufuli amlilia
Waziri Mkuu wa Urusi aambukizwa corona, awekwa karantini