Uongozi wa Mwadui FC amekanusha tuhuma zilizotolewa na aliekua kocha mkuu wa timu hiyo Khalid Adam, kuhusu kunyimwa fedha za usajili wa wachezaji, wakati wa maandalizi ya Ligi Kuu msimu huu 2020/21.

Khalid ambaye alitangaza kubwaga manyanga ndani ya klabu hiyo ya mkoani Shinyanga, alirusha tuhuma hizo kwa uongozi saa chache kabla ya kutangaza maamuzi ya kuondoka klabuni hapo.

Mwenyekiti wa klabu Mwadui FC Nurdin Suleiman, amesema hakuna ukweli juu ya tuhuma hizo, na kilichofanywa na kocha Khalid ni kutaka kuwachafua baada ya kushindwa kufanya kazi yake kwa usahihi.

“Sidhani kama alikosa pesa ya usajili na suala kama hili ni letu kati yeye na sisi, hivi vipo ndani ya wajumbe.” Amesema Nurdin.

Kuhusu kulipwa mshahara wa mwezi mmoja tu mpaka sasa, mwenyekiti huyo alisema kuwa hana uhakika, lakini atakapokabidhiwa rasmi ofisi na makabrasha yote, ndipo anaweza kujua kama hilo lipo au la.

“Kama unavyofahamu mimi nimeteuliwa kushika jukumu hili siku kadhaa zilizopita, sijaingia ofisini rasmi, ninakuahidi nitakapokabidhiwa kila kitu nitafanya kazi ya kulichunguza hili la mishahara ya wachezaji, ili kubaini kama kuna ukweli wa kulipwa mwezi mmoja pekee.” Amesema Nurdin.

Songombingo la uongozi wa Mwadui FC kurushiwa tuhuma za kushindwa kuonesha ushirikiano na benchi la ufundi wakati wa usajili, limeibuka kufuatia kikosi cha klabu hiyo kukubali kichapo cha mabao 5-0 dhidi ya Young Africans Jumamosi (Desemba 12), Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga.

Mwadui FC imekuwa timu pekee Ligi Kuu iliyokubali kufungwa mabao mengi, ilichapwa mabao 6-1 dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Oktoba 25, mwaka huu, na Oktoba 30, ikabugizwa 5-0 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Tanzia: Mzee Jengua afariki dunia
Wanafunzi 59 wadakwa na simu kwenye chumba cha mtihani