Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC unatarajia kukutana na Nahodha na Mshambuliaji wa kikosi cha klabu hiyo John Raphael Bocco.

Mpango huo umeendaliwa makusudi na Viongozi wa Simba SC, kufuatia kiwango cha Mshambuliaji huyo kuporomoka tofauti na ilivyokua misimu iliyopita ambapo alionesha kuisaidia klabu hiyo kwa kupachika mabao muhimu na ya ushindi.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Simba SC Ahmed Ally amesema Bocco atakutana na viongozi ili kujadiliana mambo kadhaa ambayo huenda yakasaidia kumrudisha kwenye kiwango chake kama ilivyozoeleka.

“Bocco amekua na wakati mbaya sana msimu huu, lakini sina maana kama hana uwezo kisoka, lakini inafahamika kuwa huyu ni binaadamu na huenda akawa na mambo tofauti ambayo yanamvuruga kwa sasa.”

“Uongozi umeona kuna haja ya kukutana naye, ili kujua tatizo lipo wapi na kuweza kumsaidia, na aweze kurejea kwenye kiwango chake na kuisaidia Simba SC.” Amesema Ahmed Ally.

Mpaka sasa Bocco hajafunga bao tangu msimu huu 2021/22 ulipoanza na hapati nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha Simba SC, zaidi ya kutumika kama mchezaji wa akiba.

Kocha Gabon atoa ufafanuzi
Kisubi Out, Mtibwa Vs Simba SC