Chama kikuu cha upinzani nchini Rwanda cha Democratic Green Party, kimefanikiwa kushinda ubunge kwa mara ya kwanza katika historia ya vyama vingi nchini humo.

Chama hicho ambacho ndicho chama pekee cha upinzani kilichosajiliwa kinachoshiriki chaguzi hizo, kimefanikiwa kushinda nafasi mbili za ubunge katika uchaguzi wa ubunge uliomalizika wiki hii.

Aidha, chama tawala cha Rwanda Patriotic Front (RPF-Inkotanyi) kimefanikiwa kuzoa viti 40 kati ya 53 vya ubunge wa kuchaguliwa, ikipata asilimia 74 ya kura zote.

Vyama vingine ambavyo ni vyama washirika vya chama tawala cha RPF, Social Democratic Party imepata asilimia tisa ya kura zote na kufanikiwa kuwa na nafasi tano bungeni. Chama kingine cha Liberal Party (mshirika wa chama tawala) kimepata asilimia saba sawa na nafasi nne za wabunge.

Tofauti na nchi nyingi, nchini Rwanda watu hupiga kura kuchagua vyama badala ya mtu anayesimamishwa na chama. Baada ya uchaguzi, vyama vilivyopata asilimia kubwa ambayo ni kuanzia asilimia tano huwateua makada wao kuwa wabunge kwa idadi inayotokana na asilimia hizo walizopata.

Kutokana na historia hiyo ya ushindi, kiongozi wa chama hicho cha upinzani, Frank Habineza alieleza kufurahishwa na ushindi huo.

Frank Habineza

“Ni mara ya kwanza tumeweza kuwa na wabunge wa chama cha upinzani kwa kipindi cha miaka 24 sasa. Ni hatua nzuri ambayo inafungua ukurasa mzuri wa kidemokrasia nchini Rwanda,” The East Africa inamkariri Habineza.

Aliahidi kuwa chama chake kitafanya kazi ya kuisimamia Serikali bungeni, na kwamba wanapanga kugombea nafasi ya Uspika wa bunge.

Wakosoaji wa Rais Paul Kagame, wamekuwa wakimlaumu kuwa analidhibiti Bunge na kuhakikisha linafanya kile ambacho Serikali inataka, ikiwa ni pamoja na kupitisha sera na sheria kwa matakwa yake.

Tume ya uchaguzi nchini humo imesema kuwa itaendelea kutoa matokeo ya uchauzi wa viti maalum vya wanawake.

TCRA yataka wateja wa DSTV, AZAM na ZUKU waliolipishwa kuwasilisha taarifa zao
Wanajeshi 10 wahukumiwa kwa tuhuma za ubakaji