Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Edwin Mwanzinga ameikingia kifua halmashauri hiyo kutokana na taarifa ya upotevu wa fedha shilingi bilioni 5.5 za ujenzi wa stendi mpya ya halmashauri hiyo inayojengwa katika eneo la Mji Mwema Mjini Njombe.

Akizungumza na Dar24Media mkoani humo, Mwanzinga amesema kuwa ameshangazwa na tuhuma hizo dhidi ya baadhi ya watumishi akiwemo Ofisa masuhuli kwa kuwa ameisoma taarifa ya mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali hivyo hakuna mahali ilipoonyesha moja kwa moja kuna upotevu wa fedha hizo.

“Ile ripoti kwa ujumla wake mimi nimeisoma na kuzipitia hoja zote na kimsingi katika hoja zile hakuna mahali walipoonyesha moja kwa moja kuna upotevu, na hoja ya kwamba bilioni tano na nusu zimepotea kwa akili ya kawaida tu stendi isingekuwepo kwasababu stendi ile tunatumia karibu 5.7 bilioni,”amesema Mwanzinga

Amesema kuwa anakubaliana na hoja ya kucheleweshwa kwa mradi upande wa mkandarasi pamoja na halmashauri kwa kuwa mkurugenzi alikuwa akipokea maelekezo ya kuendelea na mkandarasi wa zamani aliyeshindwa kuendelea na mradi huo huku akipata maelekezo kutoka kwa viongozi wa ngazi ya mkoa,hivyo watumishi hao walikamatwa kwa kuonewa.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ramadhani, George Sanga amesema kuwa tatizo kubwa kwa halmashauri hiyo ni mambo mengi yamekuwa yakiishia kwenye kamati ya fedha na wengine kushindwa kuonekana kama sehemu ya maamuzi.

Aidha, siku za hivi karibuni mkuu wa mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wote waliotajwa katika ripoti ya mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali kwa tuhuma za kusababisha upotevu wa kiasi cha shilingi 5.5 bilioni za ujenzi wa stendi mjini Njombe

 

 

 

Video: Maalim Seif rasmi ACT, Mbuge mwingine upinzani matatani
Polepole asema Maalim Seif ni fundisho