Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) Salum Hashim Salum, amechukua fomu kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwania Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hashimu alikabidhiwa fomu hiyo na katibu mkuu wa Idara ya Organization ya CCM Galous Nyimbo, na kutakiwa kutafuta wadhamini 250 katika mikoa ya Zanzibar ukiwemo wa Pemba.

Mapema akizungumza na waandishi wa habari, Salum alisema akichaguliwa kuwa Rais wa serikali ya mapinduzi (SMZ), anakusudia kutoa kipaumbele kwenye sekta ya michezo Zanzibar, ikiwemo mpira wa miguu na kuhakikisha unapata udhamini utakaoinua mchezo huo.

“Mimi ni mchezaji wa soka wa zamani na kiongozi wa mpira wa miguu, nakusudia kuimarisha soka ili liweze kutoa ajira kwa vijana hapa Zanzibar.” alisema.

Salum alikua wanachama wa 24 wa CCM kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kupitishwa kuwa mgombea wa chama hicho tawala kwa nafasi ya Urais.

Baadhi ya wanachama wa CCM waliochukua fomu za kuomba ridhaa ya kuwania Urais Zanzibar kupitia chama hicho ni Mwantum Mussa Sultan, Mbwana Bakari Juma, Ali Abeid Karume, Mbwana Yahya Mwinyi, Dkt. Hussein Mwinyi, Omar Sheha Mussa, Shamsi Vuai Nahodha, Mohamed Hija Mohammed, Mohammed Jaffar Jumanne na Balozi Meja Jenerali Mstaafu Issa Suleimani Nassor.

Rais ampongeza bilionea mpya wa madini
Kamati ya nidhamu TFF yawahukumu Morrison, Mkude