Tunaendelea kulimulika Kundi C, ambapo leo tuko na Denmark inayozungukwa na wanafamilia wengine wa kundi hilo ambao ni timu za Ufaransa, Australia na Peru.

Kufuzu:

Licha ya kufuzu kwa mara ya kwanza katika fainali za kombe la dunia, tangu walivyofanikiwa mwaka 2009 kwa ajili ya fainali za mwaka 2010, ikiwa ni takribani miaka nane, mashabiki wa soka nchini Denmark wamerejesha mapenzi na imani kubwa kwa timu yao.

Kimahusiano, hali ilikuwa mbaya baina ya timu hiyo na mashabiki, baada ya kikosi cha Denmark kushindwa kufuzu fainali za mwaka 2014 zilizochezwa nchini Brazil.

Katika kampeni za kuwania kufuzu fainali za mwaka huu, Denmark ilipangwa katika kundi E (Kundi la sita), ukanda wa barani Ulaya (UEFA), lililokuwa na timu za Poland (Alama 25), Montenegro(Alama 16), Romania (Alama130, Armenia (Alama 7) na  Kazakhstan (Alama 3) na Denmark yenyewe (Alama 20).

Alama hizo hazikutosha kwa taifa hilo lenye idadi ya watu 5,748,769, kufuzu moja kwa moja kwenye fainali za kombe la dunia, walilazimika kucheza mchezo wa mtoano dhidi ya Jamuhuri ya Ireland.

Mchezo wa mkondo wa kwanza kwa timu hizo ulichezwa Parken Stadium, mjini Copenhagen na kumalizika kwa matokeo ya sare ya bila kufungana, huku mchezo wa mkondo wa pili uliofanyika Aviva Stadium, mjini Dublin, Denmark walichomoza na ushindi wa mabao matano kwa moja.

Mabao hayo yalifungwa na Andreas Bødtker Christensen dakika ya 29, Christian Dannemann Eriksen dakika bya 32, 63, 74 na Nicklas Bendtner akafunga bao la tano kwa mkwaju wa penati dakika ya 90.

Bao la kufutia machozi kwa Jamhuri ya Ireland lilifungwa na Shane Patrick Michael Duffy katika dakika ya 6.

Majina ya utani ya timu ya taifa ya Denmark: De Rød-Hvide (The Red-White) na Danish Dynamite

Mfumo: Kikosi cha Denmark hutumia mfumo wa 4-3-3.

Related imageMchezaji Nyota: Christian Eriksen (Tottenham Hotspur).

Related imageMchezaji hatari: Thomas Delaney (Werder Bremen).

Image result for Simon Thorup Kjær - denmarkNahodha: Simon Thorup Kjær (Sevilla CF)

Image result for Åge Fridtjof HareideKocha: Åge Fridtjof Hareide (64), raia wa Norway.

 

Ushiriki: Denmark imeshiriki fainali za kombe la dunia mara nne (4). Mwaka 1986, 1998, 2002 na 2010.

Mafanikio: Kufika hatua ya robo fainali (1998).

 

Kuelekea 2018:

Kocha Åge Fridtjof Hareide  atakuwa na kila sababu ya kuweka rekodi ya kipekee ya kuivusha Denmark katika hatua ya robo fainali ambayo ndio rekodi kubwa kwa taifa hilo tangu walipoanza kushiriki fainali za kombe la dunia mwaka 1986.

Kocha huyo amekuwa na imani kubwa na kikosi chake, tangu akiwa katika mchakato wa kusaka nafasi ya kushiriki fainali za mwaka huu.

Mchezaji anaempa jeuri kocha huyu ni Christian Eriksen ambaye amekuwa na msimu mzuri, akicheza katika klabu ya Tottenham Hotspur ya England.

Mara kadhaa wakati wa michezo ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia, Christian Eriksen alionesha ushirikiano mkubwa na wachezaji wenzake na kuleta mafanikio ya kufuzu fainali za kombe la dunia.

Christian Eriksen tayari ameshafikia rekodi iliyowekwa na mchezaji wa zamani wa Denmark Michael Laudrup ya kufunga mabao 11 katika michezo 12.

“Fainali za kombe la dunia zinastahili kutumikiwa na mchezjai kama huyu,” aliwahi kusema kocha Age Hareide. “Naamini tutakuwa tishio kwa timu nyingine, kwa sababu tuna mchezaji kama Christian Eriksen.”

Wachezaji wengine ambao ni shupavu katika kikosi cha Denmark ni kiungo Thomas Delaney, ambaye anashika nafasi ya pili kwa ufungaji wa mabao katika kikosi cha timu hiyo, Washambuliaji Nicolai Jorgensen, Andreas Cornelius na Nicklas Bendtner.

Sehemu ya ulinzi (Beki) kuna watu kama Brentford, Andreas Bjelland na nahodha Simon Kjær.

Denmark itaanza kampeni za kuusaka ubingwa mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Peru, Uwanja Mordovia, mjini Saransk, Juni 16, kisha watapambana na Australia Juni 21, Uwanja wa Cosmos, mjini Samara, na mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi watakutana na Ufaransa Juni 26, Uwanja Luzhniki, mjini Moscow.

Je, Denmark watachomoza katika msitu huu wa kundi C? Macho na masikio yetu yatashuhudia sauti na picha kutoka Urusi, Dar24 itakusogeza pia karibu na taifa ili uyafahamu yanayojili kwenye fainali hizo.

Kesho tutaimulika tena timu nyingine, kaa hapahapa.

972.7 Milioni zakusanywa kwa makosa ya usalama barabarani
Video: Kinana ajiuzulu, majina wezi wa CCM sasa yaanza kuvuja