Tunaanza kulichambua kundi H lenye timu za Poland, Senegal, Colombia na Japan huku mashabiki wa soka duniani wakihesabu muda kabla ya kuanza kwa fainali za kombe la dunia nchini Urusi hapo kesho.

Kundi hili ni la mwisho katika uchambuzi wa makundi yote tuliokuletea wewe msomaji wetu, kupitia tovuti yako pendwa na Dar24.

Tunaanza na timu ya taifa ya Poland ambayo ni sehemu ya mataifa 13 ya barani Ulaya (UEFA) yaliyofuzu kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka huu, ambayo yaliongoza misimamo ya makundi yao, na kufuzu moja kwa moja.

Katika mchakato wa kuwania kufuzu fainali za mwaka huu, Poland walipangwa kundi E (Kundi La Tano) lililokua na timu za mataifa Denmark, Montenegro,        Romania, Armenia na Kazakhstan.

Taifa hilo lenye watu zaidi ya 38,422,346  liliongoza msimamo wa kundi hilo kwa kufikisha alama 25 ikiwaacha Denmark waliomaliza katika nafasi ya pili kwa kuwa na alama 20, Montenegro (Alama 16), Romania (Alama 13), Armenia (Alama 7) na Kazakhstan waliburuza mkia kwa kuwa na alama 3.

Jina la utani la timu ya taifa ya Poland: Biało-czerwoni (The White and Reds).

Mfumo: Kikosi cha Poland hutumia mfumo wa 4-2-3-1.

Image result for Robert Lewandowski - PolandMchezaji Nyota na Nahodha: Robert Lewandowski (Bayern Munich)

Image result for Piotr Zielinski - PolandMchezaji hatari: Piotr Zielinski (Napoli)

Image result for Adam Nawalka - PolandKocha: Adam Nawalka (60), raia wa Poland.

Ushiriki: Poland imeshiriki fainali za kombe la dunia mara saba (07). Mwaka 1938, 1974, 1978, 1982, 1986, 2002 na  2006

Mafanikio: Mshindi wa tatu (1974, 1982)

 

Kuelekea 2018:

Kocha Adam Nawalka hatokua na jambo la ziada, zaidi ya kutaka kuivusha Poland na kuifikisha hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la dunia kwa mwaka huu, ili kuifikia rekodi ambayo kwa mara ya mwisho iliwekwa mwaka 1974 na 1982.

Katika miaka hiyo Poland ilifika hatua ya nusu fainali na ilishindwa kuingia fainali na hatimae kucheza mchezo wa kumsaka mshindi wa tatu.

Kocha Nawalka ana nia kubwa ya kuifikia rekodi hiyo, lakini kwanza ameshaeleza wazi, hitaji lake la kutaka kufika robo fainali na kisha ataangalia kama atakua na uwezo wa kuingia nusu fainali na ikiwezekana fainali.

Kasi ya kocha huyo iliyokiwezesha kikosi cha Poland kushinda michezo 10 wakati wakiwania kufuzu fainali za mwaka huu, ndio anayoitarajia watakapokua nchini Urusi.

Tegemeo lake kubwa ni nahodha na mshambuliaji Robert Lewandowski, ambaye tayari ameshavunja rekodi kwa kufunga mabao 16 katika michezo ya kuwania kufuzu, na kumfanya afikishe rekodi ya mabao 52 aliyofunga akiwa na timu ya taifa.

Wachezaji wengine wanaompa matumaini makubwa kocha Nawalka ni mlinda mlango Wojciech Szczesny, Kamil Glik, Grzegorz Krychowiak na Kamil Grosicki.

Poland wataanza kampeni za kuusaka ubingwa wa mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Senegal, Uwanja wa Otkritie mjini Moscow Juni 19, kisha watapambana na Coombia Juni 24, Uwanja wa Kazan mjini Kazan, na mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi watakutana na Japan Juni 28,uwnaja wa  Volgograd mjini Volgograd.

Usikose na usiache kuendelea kufuatilia makala hizi, kesho tutaendelea kumulika timu za kundi hili. Nakukumbusha tena kuendelea kufuatilia channel yetu ya YouTube ya Dar24 Media.

TCRA yatoa mbinu kukabiliana na wezi wanaotoa namba ya simu kutumiwa pesa
Makala: Wachezaji wenye umri mdogo zaidi watakaowasha moto Urusi