Jeshi la Urusi limefanya mashambulizi na kuteka meli tatu za Ukraine katika eneo la Rasi ya Crimean, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Meli mbili za mizigo na moja iliyokuwa inazisindikiza zimewekwa chini ya ulinzi, huku wafanyakazi kadhaa wa meli hizo wakiripotiwa kujeruhiwa. Urusi inadai Ukraine ilingia katika eneo lake ndani ya bahari hiyo.

Tukio hilo linaloongeza uhasama kati ya nchi hizo mbili, limetokea wakati ambapo Ukraine ikitarajia kupiga kura leo kupitisha matumizi ya sheria za kijeshi.

Aidha, Urusi imeweka meli kubwa ya mizigo iliyoziba daraja katika eneo la Kerch Strait, ambalo ndiyo njia pekee ya kuingia kwenye bahari ndogo ya Azov, inayotumiwa na nchi hizo mbili.

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama la Taifa la Ukraine, Rais wa nchi hiyo, Petro Poroshenko amekaririwa akitaja vitendo vya Urusi kama uchokozi wa kiwendawazimu.

Urusi imetuma ombi la kuitishwa kwa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambapo Balozi wa Marekani katika Baraza hilo, Nikki Haley amesema kimeitishwa kufanyika leo majira ya saa tano asubuhi jijini New York, kwa saa za Marekani.

Taharuki kati ya Urusi na Ukraine katika eneo la Bahari Nyeusi na Bahari ya Azov, katika eneo la Rasi ya Crimean ilizuka tangu mwaka 2014.

Boti yazama ziwa Victoria ikiwa na abiria 90 wakisherehekea
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Novemba 26, 2018

Comments

comments