Aliyekua bingwa wa mbio fupi duniani Usain Bolt, amekiri kufurahishwa na mwenendo wa majaribio ya soka lake la kimataifa, akiwa na klabu ya Central Coast Mariners ya Australia.

Bolt ambaye alianza kutamba katika mbio fupi duniani mwaka 2008, tayari ameshacheza michezo miwili ya majaribio akiwa na klabu hiyo, ambayo imejitolea kumsaidia kwenye ndoto zake za kutaka kuwa mchezaji hodari wa mchezo wa soka.

“Kwa hakika ninafurahia maisha ya mchezo wa soka, tangu nimekuja hapa ninafurahishwa na ninachojifunza, kwa muda mfupi nimejifunza mambo mengi sana na nimeanza kuyatumia ninapokua uwanjani,” alisema Bolt alipohojiwa na mwandishi wa habari wa tovuti ya klabu hiyo.

“Mpango wangu ni kutimiza ndoto za kucheza soka katika hadhi ya juu, ninaamini hakuna kitakachoshindikana, kila hatua ninayoipitia ninajifunza na ninaamini nitaweza, kama ilivyo kwa wachezaji wengine ambao wamedumu kwa muda mrefu kwenye mchezo huu pendwa duniani.

“Tayari nimeshacheza kwa dakika 45 dhidi ya North Shore, dakika 10 za mwisho nilijihisi kuchoka sana, lakini nilijilazimisha na nilifanikiwa kumaliza salama.”

“Ninajihisi kubadilika sana kimwili tangu nilipoanza mazoezi na kikosi cha timu hii, ninamshukuru kila mmoja hapa, nimekua nikipata ushirikiano wa hali ya juu, na wakati mwingine ninajiuliza kwa nini nisingefanya maamuzi mapema ya kuhamia katika mchezo wa soka.”

Kwa upande wa kocha wa klabu ya Mariners Mike Mulvey amesema: “Usain anaendelea vizuri na amekuwa mwepesi wa kujifunza, ninaamini akiwa hapa kwa kipindi kirefu ataweza kutimiza lengo lake.”

“Kwa kumsaidia na kufikia hatua ya kuwa mchezaji mzuri, anahitaji muda wa miezi 12 (mwaka mmoja) wa kijifunza mambo mbalimbali anapokua uwanjani, sina shaka atafanikiwa.”

Nyuki 20,000 wazua tafrani kwenye ndege
Carlo Ancelotti hajui nani ataikabili Juventus

Comments

comments