Uongozi wa klabu ya Olympiakos ya Uguriki umeshindwa kutoa tamko lolote, baada ya kuhusishwa na mpango wa kutaka kumrudisha kiungo kutoka Ivory Coast, Yaya Toure.

Toure, ambaye kwa sasa ni mchezaji huru, baada ya kuachwa na mabingwa wa soka nchini England Man City mwishoni mwa msimu uliopita, amekua katika harakati za kusaka klabu ya kuichezea.

Jana Jumatano, wakala wake Dimitry Seluk, alithibitisha mteja wake kufanyiwa vipimo vya afya jijini London, na kueleza uwezekano wa mchezaji huyo kucheza soka jijini humo.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 35, aliwahi kuitumikia klabu ya Olympiakos kwa msimu mmoja (2005-06) na kisha alisajiliwa na AS Monaco  ya Ufaransa, kabla ya kutua kwa mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona.

Meneja wa klabu ya Olympiakos Pedro Martins, ambaye kikosi chake kitaikabili Burnley leo usiku katika mchezo wa kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Europa League, alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kumsajili Toure hakutaka kuzungumza lolote kuhusu mchezaji huyo.

“Nina wachezaji wenye uwezo wa kucheza soka kwa msimu mzima, suala la kuongeza mchezaji mwingine ama kutokuongeza linategemea na mipango ya baadae, lakini kama itawezekana nitafanya hivyo.” Alisema Pedro Martins.

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa kwenye uwanja wa Turf Moor Olympiakos walikubali kuchapwa bakora tatu kwa moja dhidi ya Burnley, na kama watahitaji kusonga mbele wanatakiwa kusaka ushindi wa mabao mawili kwa sifuri ama zaidi.

Mgombea mmoja wa Udiwani aenguliwa
Lucas Moura kurudisha heshima Tottenham Hotspurs