Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA) kimemfukuza uanachama diwani wa kata ya majengo wilaya ya Sumbawanga, Dickson Mwanandenje

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Chama hicho mkoa wa Rukwa, Shadrack Malila ambapo amesema kuwa Baraza kuu la CHADEMA mkoa wa Rukwa lililokutana limeridhia kwa kauli moja kumfuta uanachama diwani huyo kwa kile kilichoelezwa ni usaliti ndani ya chama.

Amesema kuwa diwani huyo hivi karibuni alionekana kwenye mkutano wa hadhara wa mbunge wa Sumbawanga mjini CCM, Aeshi Hilaly na kupewa nafasi ya kupanda jukwaani ambako alimsifia mbunge huyo pamoja na chama chake (CCM).

“Kwanza alitoka kwenye Kata yake na kwenda hadi Kata ya (Mazwi) ambako mkutano huo ulifanyika, pili akaomba nafasi ya kuongea na kumsifia mbunge huyo akidai ameleta maendeleo ndani ya jimbo kitu ambacho si kweli na sisi kwa tukio hilo tumeona ni usaliti tosha alioufanya hivyo hastahili kuendelea na sisi,”amesema Malila

Hata hivyo, Malila ameongeza walikuwa na taarifa za diwani huyo kutaka kuhamia CCM hivyo wamempa njia ya kwenda bila kujinadi kuwa ameondoka, huku wakiendelea na uchunguzi juu ya diwani mwingine wa CHADEMA ambaye naye anatuhumiwa kuwa miongoni mwa wasaliti na ikithibitika naye watamfuta uanachama.

 

Video: Ngome ya Lowassa Monduli yavunjika, Maalim Seif, Lowassa watikiswa
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Agosti 12, 2018