Baada ya kuibamiza Mtibwa Sugar mabao 3-2, Kocha Mkuu wa KMC FC Hitimana Thiery amefichua siri ya ushindi huo ulioiwezesha klabu yake kufikisha alama 27, katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Miamba hiyo ilikutana jana Alhamis (Mei 12) Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, huku Mtibwa Sugar wakipata mabao yao kupitia kwa George Makang’a na Ismail Muhesa, mabao ya KMC FC yalifungwa na Matheo Anton aliyefunga mabao mawili na lingine likapachikwa wavuni na Hassan Kessy.

Kocha Hitimana amesema wakati wa mapumziko aliwaambia wachezaji wake wanapaswa kujiamini kwani walikua na dakika nyingine 45 za kipindi cha pili.

Amesema alitumia mfanyo wa Real Madrid wakati ikicheza mchezo wa Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Manchester City, kusisitiza ujumbe wake kwa wachezaji wa KMC FC na mwisho wa dakika 90 mambo yaliwanyookea.

“Tulikwenda mapumziki tukiwa nyuma kwa mabao mawili, nilipoingia ndani niliwaambia bado wana dakika nyingine 45 za kubadilisha matokeo, niliwapa mfano wa juzi tu hapa, Real Madrid na Man City nakumbuka hadi dakika ya 89 City alikua ana nafasi, lakini hadi dakika ya 98 matokeo yaligeuka na Real akapita.”

“Tulifanya makosa mawili ambayo yalitusababishia kufungwa mabao, na hatukutoa nafasi nyingine kwa wenzatu kutufunga, nashukuru wachezaji wangu walinielewa na wamefanikiwa kuondoka na alama tatu.”

“Tukubali tu mchezo ulikua mzuri naamini hata mpinzani wetu angekua na mchezo mzuri na yeye angeweza kushinda mchezo huo, kwa hiyo siwezi kukwambia kuwa ilikua miujiza ni Mungu tu ametupatia ushindi huu baada ya kuona vijana wangu walionyesha bidii kipindi cha pili.” amesema Kocha Hitimana

Kupoteza mchezo dhidi ya KMC FC kunaifanya Mtibwa Sugar kuendelea kuwa na alama 27 zinazoiweka kwenye nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mtibwa Sugar: Tutabaki Ligi Kuu, hatushuki
Simba SC yashtukia vita ya ubingwa 2021/22