Aliyekua meneja wa klabu bingwa barani Ulaya Real Madrid Julen Lopetegui, ameanza kuhusishwa na taarifa za kuwaniwa na shirikisho la soka nchini Marekani (USSF), ili akabidhiwe mikoba ya kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo.

Taarifa zilizotolewa na tovuti ya AS zinadai kuwa, viongozi wa shirikisho la soka nchini Marekani wameanza kumjadili Lopetegui ambaye kabla ya kuwa meneja wa Real Madrid, alikua kocha mkuu wa timu ya taifa ya Hispania.

Tangu kocha Bruce Arena alipondoka mwaka 2017, kikosi cha Marekani kimekua chini ya kocha wa muda Dave Sarachan, na viongozi hao wameona ni wakati muafaka wa kumsaka mkuu wa benchi la ufundi la timu hiyo.

Hata hivyo bado Lopetegui hajakutana uso kwa uso na viongozi wa shirikisho la soka nchini Marekani kwa ajili ya kuanza mazungumzo, lakini inaelezwa wakati wowote pande hizo mbili huenda zikakutana.

Kikosi cha timu ya taifa ya Marekani hakikufanya vizuri katika michezo ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya England na Italia iliyochezwa juma lilolopita, hali ambayo imeendelea kutoa msukumo wa kusakwa kwa kocha mkuu, ambaye ataweza kurejesha furaha kwa mashabiki wa soka nchini humo.

Marekani haikufanikiwa kushiriki fainali za kombe la dunia 2018 zilizofanyika nchini Urusi, baada ya kushindwa kufanya vyema kwenye michezo ya kuwania kufuzu.

Endapo Lopetegui akakabidhiwa kikosi cha Marekani, kazi kubwa itakua ni kuhakikisha anaipeleka kwenye fainali za kombe la dunia za 2022 zitakazofanyika nchini Qatar, sambamba na kufanya vyema kwenye fainali za mataifa bara la Amerika ya kati na kaskazini itakayofanyika 2019.

Andres Iniesta: Dembele ana uwezo mkubwa
N'Golo Kante kuweka rekodi Stamford Bridge