Wakati Serikali za nchi nyingi Afrika zikifanya juhudi kubwa kupambana na ndoa za utotoni na mapenzi katika umri mdogo, hali ni tofauti nchini Japan ambapo utafiti umebaini kuwa asilimia 42 ya wanaume na wanawake ambao wamefikia umri wa ‘utu uzima’ hawajawahi kufanya mapenzi.

Hayo yamebainika kupitia utafiti uliofanywa hivi karibuni na Taasisi ya Taifa ya Japan ya Idadi ya Watu na Hifadhi ya Jamii ambao hufanywa kila baada ya miaka mitano kuhusu changamoto za kijamii zinazolikabili taifa hilo.

Imebaini kuwa kati ya wananchi wake wenye umri kati ya miaka 18 hadi 34, ni asilimia 58 pekee ambao tayari wameshawahi kufanya tendo la ndoa na kwamba watu huchelelewa kujihusisha na mahusiano ya mapenzi na hata kufunga ndoa. Imebaini pia kuwa baadhi yao hawana mpango kabisa wa kufunga ndoa.

Utafiti huo umeonesha ongezeko la watu ambao ni bikira hadi kufikia umri wa utu uzima ukilinganisha na mwaka 2010 ambapo utafiti ulionesha asilimia 36.2 ya wanaume na 38.7 ya wanawake ndio walioeleza kuwa ni bikira.

warembo-wa-japan

Kutokana na matokeo hayo, Serikali ya Japan imekuwa ikihamasisha wananchi kufunga ndoa ili kuepuka kuporomoka kwa idadi ya watu ambao ni nguvu kazi ya taifa hilo. Serikali hiyo imekuwa ikitoa ruzuku kwa wanandoa pamoja na kuwapunguzia kodi katika baadhi ya masuala yanayohusu moja kwa moja familia katika jitihada za kuwahamasisha wengine kuingia katika ndoa.

“Asilimia 30 ya wanaume waliofanyiwa utafiti na asilimia 26 ya wanawake walioshiriki utafiti huo walieleza kuwa hawana mpango wa kujihusisha na masuala ya mahusiano hivi kwa wakati huu” utafiti huo ulibainisha.

Mourinho Na Guardiola Kukutana Tena Mwezi Oktoba
Video: Waziri Makamba atoa onyo kwa wanaotupa hovyo taka ngumu