Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Twaweza umebaini kuwa asilimia 91 ya wananchi wanapinga kipengele cha sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 kinachoipa Mamlaka Serikali kulifungia gazeti bila kuhoji.

Utafiti huo wa Twaweza uliofanywa kati ya tarehe 10 na tarehe 25 Februari 2016 pia umebainisha kuwa asilimia 78 ya wananchi wanaamini kuwa upatikanaji wa habari hupunguza vitendo viovu ikiwa ni pamoja na rushwa.

Imebainika pia kuwa asilimia 60 ya wananchi wanataka Serikali iwe na Mamlaka ya kuzuia habari ambazo zina umuhimu kwa usalama wa taifa pekee.

Utafiti huo uliowafikia watu 1,811 kutoka maeneo mbalimbali Tanzania Bara, ulibaini kuwa bado wananchi wanaamini zaidi redio kwa kupata habari kuliko vituo vya runinga, magazeti na mitandao ya kijamii.

Redio inaaminika na asilimia 80 ya wananchi na runinga inaaminika na asilimia 73 ya wananchi, tofauti na magazeti yanaaminika kwa asilimia 27 tu ya wananchi.

Ingawa mitandao ya kijamii inatumiwa na asilimia 47 ya watu Tanzania Bara, wanaiamini kwa kiasi kidogo sana kama chanzo cha habari.

Utafiti huo umepewa jina la “Mwangaza, Wananchi na Haki ya kupata habari”.

Zitto Kabwe atema Cheche Bungeni, aing'ang'ania Takukuru
Justin Bieber ajibu tuhuma za kujifananisha na Mungu