Utajiri wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Fellowship, Zachary Kakobe umegeuka habari nyingine baada ya kuhojiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa mujibu wa kiongozi huyo wa kanisa.

Akizungumza hivi karibuni katika ibada kanisani kwake jijini Dar es Salaam, Askofu Kakobe alieleza kuwa amehojiwa na TRA na kufanyiwa ukaguzi na kwamba alichowaeleza kuwa anacho kimeishia kwenye pato la sadaka pekee.

TRA walitangaza uamuzi wa kumhoji Kakobe kutokana na kauli yake aliyoitoa katika ibada ya Christmas kanisani kwake kuwa ana utajiri mkubwa. Kakobe alisisitiza baadaye kuwa yeye ni tajiri wa dunia.

Askofu huyo amewaeleza waumini wake kuwa alifanyiwa mahojiano na kamati maalum iliyofika ofisini kwake ambapo aliwaeleza kuwa ana nyumba moja pekee aliyowahi kujenga ambayo ilimgharimu shilingi milioni 2 na elfu thelathini (2,030,000).

“Niliwaambia nina nyumba moja tu duniani iko Kijitonyama, nilijenga kwa gharama ya shilingi milioni 2 na kiwanja nilinunua shilingi elfu thelathini. Iko katika mtaa wa kawaida uitwao ‘Kwa Kakobe’, itafuteni mtaona nyumba yangu,” Kakobe alisimulia.

Alisema kutokana na hali hiyo, baadhi ya waumini wake waliamua kuchanga pesa miaka kumi iliyopita na kumjengea nyumba ambayo ingeweza kuwa na hadhi na mazingira mazuri anapokutana na wageni wake wa kimataifa.

Aidha, alidai kuwa aliwaeleza maafisa hao kuwa yeye na familia yake pamoja na kanisa kwa ujumla hawana mradi wowote hata wa kufuga kuku. Aliongeza kuwa yeye binafsi au mke wake hawana akaunti katika benki yoyote na sehemu yoyote isipokuwa akaunti mbili za kanisa hilo, moja ikiwa ya mfumo wa Kimataifa wa FGBF, iliyoko Meru.

Aliongeza kuwa maafisa walifanya mahojiano na familia yake pamoja na waumini kuhakikisha kama kweli hana miradi zaidi ya sadaka pekee ambazo alidai kwa wiki anaweza kupewa fedha za ‘bahasha ya sadaka ya maombi’ ambayo inaenda kwake moja kwa moja ya kiasi kisichozidi shilingi milioni 5.

Alidai kanisa halijamuajiri mtu yeyote lakini ana waumini zaidi ya 1,000 ambao hufanya kazi ya kujitolea kanisani bila kulipwa.

Kakobe anadai kuwa baada ya Kamati ya kwanza kukamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti, imetumwa kamati nyingine ambayo ilifanya pia upekuzi nyumbani kwake chumba kwa chumba.

Askofu huyo alimshauri Rais John Magufuli kuwatumbua watumishi aliodai wanafanya hivyo kwa lengo la kupanda vyeo kwani anaamini Rais ni mtu mwenye hofu ya Mungu na hakuwatuma kufanya hivyo.

“TRA kweli ndani ya sadaka?  Hii ni kweli, au kuna jambo? Alihoji. “Mimi leo nimemwaga mboga, hata Askofu [Josephat] Gwajima aliwahi kutoa mrejesho. Sasa Gwajima na Kakobe ni Mapacha,” aliongeza.

Video: Rais hataki miaka 7, lakini sisi tunataka- Cyprian
Video: Lowassa atoa maelezo mengine ziara ya Ikulu, Makonda awasha moto Dar es Salaam