Oparesheni ‘Tumbua Majipu’ inayoongozwa na Rais John Magufuli imeendelea kuzua mijadala mingi katika maeneo mbalimbali hususan pale ambapo wananchi hukutana kama maskani. Hali hii imepelekea mengi kuzungumzwa na watu kuwa na mitazamo tofauti-tofauti.

Kwa kuzingatia hilo, Paul Mwandemele, moja kati ya wananchi wa Tanzania walioingia kwenye moja kati ya maskani na kuisikia mijadala inayoendelea, amemuandikia waraka wa wazi Kiongozi huyo Mkuu wa nchi.

Usome hapa: 

Rais wangu mpendwa, nakuandikia kwa heshima kubwa. Nakupongeza kwa kazi nzuri unayoifanyia nchi yetu, hasa safishasafisha ya viongozi wabovu. Kazi hii imepokelewa vizuri na wananchi.

Hata hivyo watu wengi tunaoishi huku mitaani na kufuatilia mwendeno wa Serikali yako tumebaini mwelekeo mmoja ambao napenda nikujulishe ili hili suala lisije kukuharibia na kuharibu kazi nzuri inayofanywa.

Rais Magufuli 2

Majuzi nilikuwa kwenye mgawaha mmoja unaitwa Cruz-In Mikocheni. Wadau tuliokuwa nao walikuwa na mjadala mzito kuhusu Serikali yako. Upande mmoja wanasema Serikali yako inafukuza watu kwa ajili tu ya sifa kwa umma na kwamba kuna watu wengi wanaonewa.

Wanasema kwamba ukitaka mtu afukuzwe na Rais wewe mchafue tu kwenye vyombo vya habari, tengeneza mazingira kama hatakiwi na jamii na utaona kama Rais hatamfukuza. Kwa upande mwingine, ambao nami nimo, tulikuwa tunapinga na tunasema Rais ni mtu wa haki, anafuata sheria na ukiona mtu katimuliwa ujue uchunguzi umefanyika na uchunguzi sio lazima utangazwe na kwamba mtu huyo kapewa haki ya kuelezea upande wake. Sisi tukasema Rais ni mtu wa haki. Lakini tulibishiwa sana.

Rais wangu jamii yetu imeharibika. Watu wanafurahia wengine wakidhalilika. Watu wanapenda kuona damu. Watu wanapenda visasi. Watu wanachukiana. Wengine wanafurahia safishasafisha sio kwasababu inasaidia nchi, bali kwasababu kuna watu wanaumbuka. Kwenye vyombo vya habari na mitandaoni kuna watu sasa wanatengeneza orodha ya nani anayefuatia kwenye kuumbuliwa. Dhana ya utumbuaji majipu wanaipotosha. Visasi vyao wanataka vikamilishwe na Serikali yako. Naomba usikubali kabisa. Moja ya sifa ya kiongozi ni kutenda haki. Rais ameshika upanga mkuu na upanga huo una makali na anaweza kuutumia atakavyo. Rais wangu usikubali watu wakushinikize kuzungusha upanga kwasababu tu ya raha ya kuona kichwa kinadondoka.

Mifano ya mashinikizo haya ipo mingi. Lakini mfano wa karibuni ni wa Waziri wako, January Makamba. Lipo kundi limejiapiza kwamba lazima aanguke na tunapowasoma mitandaoni wanasema wazi kabisa namna ya kumuangusha kijana wako huyu ni kumtengenezea uchafu wa kutunga ili Magufuli aone raha kuzungusha upanga. Pamoja na kujua kabisa kwa uhakika kwamba wanayozungusha ni ya kutunga, wanajihakikishia kwamba Magufuli anaamka na upanga na akisikia tu mabaya haulizi, anakata. Lakini mimi najua huyu siye Magufuli niliyempa kura yangu. Magufuli niliyempa kura yangu ni mtu wa haki.

January Makamba

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba

Tuendelee na safishasafisha Rais wangu. Ila ni muhimu watu wanaopenda kufitiniana wajue Rais wangu ni mtu wa haki. Sio ukimsema tu kiongozi kwenye Serikali yake basi upanga unampitia. Wakijua hivyo Rais hayumbi, fitina zitapungua kwenye Serikali na kwenye siasa. Umechagua timu imara kwenye Serikali yako. Nimefurahi kwamba pamoja na mashinikizo na fitina kuhusu Prof Muhongo na Prof Maghembe bado umewapa nafasi wakusaidie. Umetengeneza sifa nzuri kwamba maneno ya magazeti na mitandaoni hayasukumi uamuzi wako.

Kuna ambao hawapendi kwamba baadhi ya watu wamo kwenye Serikali yako. Simama imara na timu yako, anayeharibu atolewe, anayesakamwa kwa fitina simama naye, utaijengea timu yako kujiamini katika kazi zao na watakufanyia kazi nzuri. Tusikubali kurudi kule kwenye miaka 10 iliyopita ambapo nchi ilipitia Mawaziri 121 kwasababu fitina ziliruhusiwa, na Mawaziri wakawa wanapukutishwa kila miezi sita. Unayo nafasi kubwa ya kuisaidia nchi kumaliza fitina kwenye siasa nchini kwa kuonyesha kwamba huchukui hatua kwa kufuata upepo, ambao zama hizi unatengenezwa mezani.

Nisamehe kama nimekukwaza kwa kutoa ushauri lakini mimi nimekupa kura yangu na ni mdau mkubwa wa kutaka Serikali yako ifanikiwe.

Abramovich Ajipanga Kumrejesha Lukaku
Florentino Perez Akalia Kuti Kavu Bernabeu