Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dar es salaam, Musa Kilakala amependekeza kupimwa kwa baadhi ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kile alichodai kuna baadhi yao wanajihusisha na matendo yasiyokuwa na maadili ikiwemo kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Tanga ya Kijani, iliyofanyika mkoani Tanga, ambapo amemuomba Spika Ndugai kama ambavyo Bunge limeazimia kupimwa ulevi kwa Wabunge, pia liwapime Wabunge ambao wanahisiwa wanajihusisha na vitendo hivyo.

Amesema kuwa kuna mkakati mkubwa wa baadhi ya Wabunge ambao wamekubaliana wa kutaka kuleta mambo yasiyofaa ndani ya nchi na lengo lao kubwa ni kutetea mapenzi ya jinsia moja.

”Napendekeza ikifika uchaguzi 2020, lazima kuna baadhi ya Wabunge wapimwe kabla hawajapewa fomu, namuomba Spika Ndugai kama ameweka vipimo vya kuwapima baadhi ya Wabunge kuhusiana na ulevi, pia aanze kuwachunguza wanaotajwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.” amesema Kilakala.

Hata hivyo, kwasasa chama hicho kinafanya kampeni ya Kijani kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na uchaguzi mkuu wa 2020.

Chanzo EATV

Masauni atoa tathmini ya hali ya usalama nchini, 'Kwasasa uhalifu umepungua'
Kanda ya Ziwa yatajwa kuwa kinara wa matukio ya ukatili kwa watoto