Vurugu kubwa zimeibuka jana katika ofisi za Umoja wa Vijana wa wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Arusha kutokana na mvutano wa mabadhiano ya ofisi kati ya Katibu aliyehamishwa, Ezekiel Mollel na Katibu mpya, Said Goha.

Vurugu hizo ziliibuka baada ya Mollel kugoma kumkabidhi ofisi Goha kwa madai kuwa anataka kutumika kama kichaka cha kuficha uozo uliofanywa na baadhi ya viongozi ili awasafishe.

Baadhi ya wanachama wa UVCCM walifika katika eneo la ofisi hizo na kuzifunga kwa makufuli wakishinikiza Mollel kuachia ofisi hiyo. Walidai kuwa kitendo cha yeye kugoma kuhama ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu na kwamba anapaswa kuchukuliwa hatua kali za utovu wa nidhamu.

“Haiingii akilini kiongozi anapata uhamisho anagoma, wewe ni nani ndani ya UVCCM?” alihoji mwanachama aliyejitambulisha kwa jina la Ibrahim Ibrahim. “Hii ni hatari sana CCM inapaswa kuliangalia hilo kwa jicho la kipekee bila kuonea mtu wala kupepesa macho,” aliongeza.

Wanachama hao pia walimlaumu Mwenyekiti wa UVCCM wa mkoa huo, Lengai Ole Sebaya kwa madai kuwa ndiye anayempotosha Mollel kwa kuifanya ofisi hiyo kama mali yake binafsi.

Hata hivyo, Mollel alipinga madai ya wanachama hao akidai kuwa waliofunga ofisi hiyo sio wanachama bali ni wahuni waliotumika.

Alisema kuwa lengo lake ni kuhakikisha haikabidhi ripoti kwa Katibu huyo mpya kwani hana imani naye, badala yake ataiwasilisha kwa mwenyekiti ya utekelezaji.

“Najua hizi ni jitihada za kujaribu kuficha madudu yanayoendelea, nitawasilisha ripoti ya kamati ambayo mimi ni mwenyekiti wa kamati hiyo lakini sio kwa katibu mpya aliyekuja ili kulinda uozo unaofanyika,” Mollel anakaririwa.

Hata hivyo, saa chache baadae, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM taifa, Shaka Hamdu Shaka alitangaza kumsimamisha kai Mollel kwa kutotii agizo halali kutoka Makao Makuu ya chama.

Shaka alisema Mollel alipewa barua ya uhamisho tangu Agosti 25 mwaka huu, akihamishiwa Makao Makuu Dar es Salaam lakini muda wote amekuwa akigoma kwa sababu zake binafsi.

Wabunge CUF wafichua ‘njama’ inayosukwa na Lipumba
Zanzibar Waandika Historia Afrika Mashariki Na Kati