Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO imesema Suala la vijana kupata ajira na kujikwamua kutoka kiuchumi baada ya janga la ugonjwa wa UVIKO-19 limeendelea kusuasua.

Ripoti hiyo iliyotolewa Agosti 11, 2022, kuelekea siku ya vijana hapo kesho, inasema hali hiyo inathibitisha kuwa UVIKO-19 iliathiri zaidi vijana kuliko marika mengine, na hususani vijana wa kike wakiathirika zaidi.

Ripoti hiyo kwa jina ‘Mwelekeo wa Ajira kwa Vijana 2022: Kuwekeza katika kurekebisha mustakabali wa vijana’ inabaini kuwa janga la UVIKO-19 limeongeza mkwamo zaidi kwenye soko la ajira hasa kwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 ambao ndio walipoteza zaidi ajira kuliko watu wazima kuanzia mapema 2020.

Hata hivyo, ripoti inasema kiwango cha vijana wasio kwenye ajira, elimu au mafunzo kwa mwaka 2020 kiliongezeka kwa asilimia 23.3, ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.5 kutoka mwaka 2019, kiwango ambacho hakijaonekana katika kipindi cha miaka 15.

“Vijana wa kike hali ni ngumu zaidi,” inasema ripoti ikionesha kuwa mwaka huu wa 2022 makadirio ya vijana wa kike watakaokuwa kwenye ajira ni asilimia 27.4 ikilinganishwa na vijana wa kiume asilimia 40.3.

“Hii ina maana vijana wa kiume wana nafasi mara 1.5 ya kuajiriwa kuliko vijana wa kike,” imesema ripoti hiyo ikitanabaisha kuwa, pengo la kijinsia ambalo limeonesha dalili ndogo kuzibika katika miongo miwili iliyopita, ni kubwa zaidi katika nchi za kipato cha chini na cha kati ikilinganishwa na zile za kipato cha juu.

“Wanachohitaji zaidi vijana ni mfumo wa soko la ajira ufanyao kazi na wenye fursa za ajira za kiutu kwa wale walioko kwenye soko, sambamba na elimu bora na fursa za mafunzo kwa wale ambao bado hawajaingia,” amesema Martha Newton, Naibu Mkurugenzi wa ILO- Sera Kuu.

Barani Afrika, kiwango cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana cha asilimia 12.7 kinaficha suala kwamba vijana wengi wamechagua kutoingia kwenye soko la ajira kabisa.

Kwa nchi za kiarabu, kiwango cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana kinaua kwa kasi na kinatarajiwa kufikia asilimia 24.8 mwishoni mwa mwaka huu.

Idadi ya vijana wasio na ajira duniani inakadiriwa kufikia milioni 73 mwaka huu wa 2022, ikiwa ni nafuu kidogo kuliko mwaka 2021 ambapo idadi ilikuwa milioni 75, lakini ripoti inasema ni ongezeko kwa vijana milioni Sita ikilinganishwa na kabla ya COVID-19 mwaka 2019.

Kenya: Mapigo ya moyo yazidi kuongezeka
Kenya: matokeo bado ni vuta nikuvute