Ukiwa mtu wa kuangalia mambo kwa juu juu basi kila kitu kwako kitakuwa kigumu. Kusoma unaweza kuona ni kugumu, kufanya kazi kugumu, hata kusubiri mshahara unaweza kuona ni kugumu.

Urahisi kwako unaweza kuwa katika kutumia pesa, pengine  na kula tu. Ila watu waerevu na wenye uvumilivu kwako kila kitu kinaweza kuwa tofauti na wewe.

Unachoona kigumu kwao wanahisi si ugumu bali ni changamoto za kuzidisha jitihada na umakini tu. Kwenye mapenzi pia hali haiko tofauti sana. Wale wanao achana kila siku si kama ndiyo wanakosewa sana kuliko wale ambao hawaachani, hapana. Suala ni lile lile tu uvumilivu.

Hakuna mapenzi duniani yanayoweza kushamiri bila suala hili. Usipokuwa na moyo wa uvumilivu katika mapenzi basi kila mtu utamuona hafai. Utakuwa mtu wa kuanzisha mahusiano mapya. Hayo si maisha sasa!

Mahusiano yaliyodumu si kwa kuwa wahusika hawakoseani au makosa wanayokoseana ni madogo sana. Hapana. Kila binaadamu ana mapungufu yake. Wote huwa wanakoseana ila tofauti yake na wengine ni kwamba busara na uvumilivu huwa msingi wa mapenzi yao na ndiyo maana tunaona wanadumu mpaka leo.

Ni binaadamu gani unaweza kuishi naye na msikoseane? Ni nani mwenye uwezo wa kukupa unachotaka kila siku? Hakuna binaadamu wa aina hiyo.

Ndiyo, kukosewa kunaumiza sana ila jiulize ni kitu gani kimetokea bila sababu? Kwenye makosa ya mpenzi wako kuna sababu nyuma yake, hebu itafute badala ya kulalamika.

Mapenzi yasiyo kuwa na uvumilivu ndani yake hayana maisha marefu. Kwa sababu binaadamu ni kiumbe mwenye kukosea.

Kuwa mvumilivu. Watu wenye hekima ni wavumilivu. Watu wenye kujielewa ni wavumilivu.

Ukiwa hauna uvumuilivu kila siku utatangaza ndoa. Leo utaachana na Mugambara kwa sababu anaongea sana na wasichana ila, jua huyo unaeenda kuwa naye anapenda sana kitu ambacho hukipendi. Anakunywa pombe je, utawezana naye? Jibu unalo.

Kumbuka, siku zote wanaovumilia ndiyo huwa wanabaki na ushindi.Bila uvumilivu Mandela asingekuja kuwa raisi wa afrika kusini.Uvumilivu ni kila kitu katika maisha.

 

Daktari ashuhudia uwepo wa Mungu kwa mgonjwa aliyechomwa mkuki mdomoni na kutokea shingoni
Bosi ndege za Serikali afariki dunia