Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), limesema kuna matarajio ya kuzalisha chanjo ya kwanza ya Malaria Duniani kwa lengo la kulinda mamilioni ya watoto dhidi ya ugonjwa huo unaogharimu maisha yao.

Chanjo hiyo inatarajiwa kutengenezwa na Kampuni moja ambayo tayari imepatiwa kandarasi, ikiwa na thamani ya takriban dola milioni 170, na itapelekea kupatikana kwa dozi milioni 18 za chanjo ya RTS,S katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, hivyo kuokoa maelfu ya maisha ya watoto kila mwaka.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Ugavi cha UNICEF, Etleva Kadilli amesema kandarasi hii inatuma ujumbe wa wazi kwa watengenezaji wa chanjo ya malaria kuendelea na kazi yao kutokana na ugonjwa huo kambao unaoambukizwa kwa binadamu kupitia mbu jike aina ya Anophelesi na licha ya ugonjwa kuzuilika na kutibika, lakini usipotibiwa unaweza kusababisha kifo.

“Tunatumai huu ni mwanzo tu na ubunifu unaoendelea unahitajika ili kutengeneza chanjo mpya na za kizazi kijacho ili kuongeza usambazaji unaopatikana, na kuwezesha soko bora la chanjo, kwani hii ni hatua kubwa katika juhudi za pamoja za kuokoa maisha ya watoto na kama sehemu ya mipango ya kuzuia na kudhibiti malaria,” amesema Kadili.

Kulingana na takwimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataaifa la Afya Duniani (WHO), zaidi ya nchi 30 zina maeneo yenye maambukizi ya wastani hadi ya juu ya malaria, huku chanjo hiyo ikitarajiwa kutoa ulinzi wa ziada kwa zaidi ya watoto milioni 25 kila mwaka.

Mapema mwezi Oktoba 2021, shirika la afya la Umoja wa Mataifa lilipendekeza matumizi yake makubwa katika nchi zenye maambukizi ya wastani hadi ya juu ya malaria, ambapo Desemba 2021, Gavi, Muungano wa Chanjo, ulichukua uamuzi wa kutoa ufadhili kwa programu za chanjo ya malaria katika nchi zinazostahiki.

Muuguzi, Janet Wanyama akimpatia chanjo ya malaria mtoto mwenye umri wa miezi tisa, katika Kliniki ya Watoto ya Hospitali ya Kaunti ya Malava Kakamega, Kenya. Picha na Gavi/2021/White Rhino Films-Lameck Orina

Chanjo ya malaria ya RTS,S ni matokeo ya miaka 35 ya utafiti na ya kwanza kuzalishwa dhidi ya ugonjwa wa Malaria, iliyozinduliwa katika programu ya majaribio ya 2019, nsa kuratibiwa na WHO, katika nchi tatu za Ghana, Kenya na Malawi ambayo imewafikia zaidi ya watoto 800,000.

Hata hivyo, Malaria inabakia kuwa moja ya ugonjwa mkubwa unaoua watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano ambapo mwaka 2020, takriban watoto nusu milioni walikufa kutokana na ugonjwa huo barani Afrika pekee, idadi ambayo ni sawa na kifo kimoja kwa kila dakika.

Inonga, Outtara kupigwa chini Simba SC
Habari kuu kwenye magazeti ya leo Agosti 17, 2022Â