Mgombea mwenza wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Martha Karua ametetea umri mkubwa wa Raila Odinga akiutaja kuwa ishara ya ukomavu na uwezo wa kuwahudumia Wakenya.

Akizungumza siku ya Jumatatu, Julai 25, katika mkutano wa kisiasa kaunti ya Kajiado, Karua amewataka wakaazi kupuuza propaganda inayoenezwa na wapinzani kuwa Raila ni mzee kiasi kwamba hatoshi kuwa rais wa tano wa Kenya.

Badala yake, aliwahimiza wakazi hao kuangazia rekodi ya Raila katika kutetea Wakenya akiwa katika serikali na upinzani na kumzawadia kwa kumpigia kura.

“Mkiambiwa Raila ni mzee, ndio ni mzee. Amekomaa na kujipanga vizuri kisiasa. Unafika wakati ambapo nchi inahitaji mtu mkomavu, anayewaza inavyostahili na asiye na hasira,” Karua alisema.

Karua aliangazia rekodi ya utendakazi ya Hayati Rais Mstaafu Mwai Kibaki akisema kuwa japokuwa alikuwa na umri mkubwa, alifanya mageuzi makubwa nchini na kuboresha pakubwa uchumi wa taifa.

Karua alisema kuwa kujitolea kwa Raila kuwahudumia Wakenya kumejaribiwa wakati akiwa kiongozi wa upinzani kwa sababu amesalia kidete katika kupigania wanyonge na demokrasia.

“Ninawaomba kuangazia rekodi ya mtu. Raila sio mnyakuzi wa ardhi na ndio maana katika kesi za unyakuzi wa ardhi ambazo wetu wengine hawawezi kukosa, yeye hajawahi kutajwa. Mchagueni Raila na muepuke viongozi ambao wanalenga kuwanyanyasa Wakenya. Matendo yana sauti kubwa kuliko maneno,” Karua alisema.

Uchaguzi Mkuu wa Kenya unatarajia kufanyika Agosti 9, 2022, ambapo Rais Uhuru Kenyatta anamaliza muda wake wa Uongozi aliohudumu kwa vipindi viwili vya Urais na duru za kisiasa zikisema dinara wa Uchaguzi huo ni Naibu Rais William Ruto na Raila Odinga.

Joslin Bipfubusa kocha mpya Polisi Tanzania
Raia wavamia kambi, Wanajeshi wajeruhiwa