Aliyekua kiungo mshambuliaji wa klabu za Tottenham na Real Madrid Rafael van der Vaart ametangaza rasmi kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 35.

Kiungo huyo ambaye pia aliwahi kuitumikia timu ya taifa lake la Uholanzi kuanzia mwaka 2001 hadi 2013, ametangaza maamuzi hayo, huku akiamini muda wa kufanya hivyo ni sasa, kutokana na kuutumikia mpira wa miguu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 25.

Akiwa na umri wa miaka 17 Van der Vaart alianza kucheza soka na kutambuliwa kimataifa akipandishwa kwenye kikosi cha wakubwa cha klabu ya Ajax Amsterdam ya nchini kwao Uholanzi.

Hadi anafikia maamuzi ya kutangaza kustaafu soka, kiungo huyo alikua na klabu ya Esbjerg ya nchini Denmark, ambayo ilimsajili mwezi August na amecheza michezo mitatu pekee, kutokana na kuwa majeruhi wa mara kwa mara.

“Haijawa rahisi kwangu kutangaza kustaafu soka, nilitamani kuendelea kucheza kwa miaka mingine mingi, lakini sina budi kufikia maamuzi haya,” aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

“Naamini mashabiki wangu wataupokea ujumbe huu kwa masikitiko, lakini sina namna zaidi ya kujiweka pembeni na kuwaangalia wenzangu wakiendeleza burudani ya soka.”

“Tumekua wote tangu nikiwa na umri wa miaka 18, kwa hakika tulifurahi pamoja na tulihuzunika pamoja, na ninaamini tutaendelea kuwa pamoja majukwaani kushuhudia burudani ya mchezo huu.”

Van der Vaart alikua sehemu ya kikosi cha Uholanzi kilichofika hatua ya fainali kwenye michuano ya kombe la dunia mwaka 2010, na kufungwa na Hispania bao moja kwa sifuri.

Akiwa na klabu ya Ajax Amsterdam alicheza michezo 117 na kufanikiwa kushinda ubingwa wa ligi ya Uholanzi (Eredivisie) mara mbili, kabla ya kutimkia nchini Ujerumani baada ya kusajiliwa na Hamburg mwaka 2005.

Van der Vaart alijiunga na mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid mwaka 2008, miaka miwili baadae alitimkia jijini London akisajiliwa na Spurs aliyoitumikia katika michezo 67 na kufunga mabao 24, mwaka 2012 alirejea Ujerumani kujiunga tena na Hamburg.

Msimu wa 2015–2016 alirejea nchini Hispania kujiunga na Real Betis ambayo aliitumikia katika michezo saba, na msimu uliofuata wa 2016–2018 alijunga na Midtjylland ya Denmark aliyoichezea michezo 17 na kufunga mabao mawili.

Daniel Arzani kukosa 2019 AFC Asian Cup
Zawadi ya Khanga kwa wajawazito yapunguza vifo vya uzazi

Comments

comments