Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Sudan ‘Falcons of Jediane’ Hubert Velud, amekanusha taarifa za kuwa mbioni kujiunga na klabu ya Young Africans, ambayo kwa sasa inamsaka mbadala wa Kocha Cedric Kaze.

Young Africans walianza mchakato wa kumsaka kocha mpya, kufuatia kumtimua kocha Kaze, baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Polisi Tanzania Tanzania uliomalizika kwa sare ya 1-1, mjini Arusha mwanzoni mwa mwezi huu.

Kocha Velud amesema taarifa za yeye kuhitajika ndani ya klabu ya Young Africans amekua akiziona na kuzisoma kwenye mitandao ya kijamii, lakini hajawahi kuzungumza na kiongozi yoyote wa klabu hiyo inayoendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 50.

Amesema kwa sasa hana lolote na kufikiria zaidi ya kukiandaa kikosi chake cha ‘Falcons of Jediane’ kuelekea michezo ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika itakayochezwa juma lijalo.

“Taarifa zote zinazosambaa mitandao ni kwamba nimefikia makubaliano na klabu ya Young Africans kutoka nchini Tanzania sio za kweli, kwa sasa nimejikita kwenye maandalizi ya kiosi cha Sudan kuelekea michezo ya kufuzu AFCON dhidi ya Sao Tome na Afrika Kusini.”

“Maandalizi yetu yanaendelea vizuri na wachezaji kutoka timu za Al Hilal na Al Merrikh wataungana na wenzao kambini hivi karibuni.Malengo yetu ni kufuzu AFCON”. Amesema Velud

Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa amewahi kuzinoa klabu za Hassania Agadir ya Morocco, ES Setif, US Alger na CS Constantine za Algeria, TP Mazembe ya DR Congo, Difaa El Jajida ya Morocco, aliyowahi kuichezea Saimon Msuva kisha kuhamia JS Kabylie ya Algeria hadi mwaka jana kabla ya kutua Sudan.

Velud ametwaa mataji kadhaa akiwa na timu alizofundisha ikiwamo Clermont ya Ufaransa aliotwaa ubingwa wa Taifa 2001-2002 kisha kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Algeria akiwa na ES Setif mwaka 2013, akabeba Super Cup nchini Algeria akiwa na USM Alger 2013 na ubingwa wa Ligi Kuu 2014 kabla ya kuhamishia makali DR Congo akiwa na Mazembe, likiwamo taji la CAF Super Cup 2016.

Al Merrikh waomba CAF iingilie kati vipimo vya Corona
Grammy yaitaja African Giant wimbo bora Afrika