Kiungo kutoka nchini Nigeria Victor Patrick Akpan ameaga rasmi kwenye klabu ya Coastal Union baada ya kuitumikia katika mchezo wa mwisho Jumamosi (Julai 02), dhidi ya Young Africans.

Coastal Union ilipoteza mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ kwa changamoto ya Penati dhidi ya Young Africans, jijini Arusha baada ya kumaliza dakika 120 kwa sare ya 3-3.

Akpan ametumia nafasi ya kuzungumza na vyombo vya habari baada ya mchezo huo na kueleza namna alivyopambana katika mchezo huo, ambao amekiri ulikua wa mwisho kwa upande wake.

Amesema alitamani kuondoka Coastal Union akiwa na kitu kikubwa alichokifanya kwa kushirikiana na wachezaji wengine, lakini haikuwa bahati kwao, na hana budi kusema kwaheri kwa kila mmoja ndani ya klabu hiyo.

“Niliumia sana kwa sababu huu ulikuwa mchezo wangu wa mwisho kuitumikia Coastal Union, nilitamani kushinda kombe hili na tulikaribia kufanya hivyo lakini tukapoteza umakini kwenye dakika za mwisho”

“Naondoka Coastal Union, siku sio nyingi mtafahamu timu ninayoelekea,” amesema Akpan

Akpan anatajwa kuwa kwenye mipango ya Klabu ya Simba SC, ambayo inaendelea kufanya usajili kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Michuano ya Kimataifa.

Inaelezwa kuwa Kiungo huyo tayari ameshasaini mkataba wa kujiunga na Simba SC kwa msimu ujao, huku wachezaji wengine wanaotajwa kuwa kwenye mpango huo ni Augustine Okrah (Ghana) Ceser Manziko (Jamhuru ya Kati, DR Congo) na Habibu Kyombo (Tanzania).

Wabunge wapambania TB
Abdul Sopu azikataa Simba SC, Young Africans