Rais John Magufuli, leo amekutana na kufanya mazungumzo na bilionea wa Nigeria, Aliko Dangote Ikulu jijini Dar es Salaam kuhusu azma yake ya kuwekeza nchini.

Dangote ambaye anamiliki kiwanda cha saruji mkoani Mtwara ameeleza kushangazwa na taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa anataka kufunga kiwanda hicho kutokana na kushindwa kumudu gharama na kutoelewana na maafisa wa Serikali.

Amemhakikishia Rais Magufuli kuwa Tanzania ni nchi yenye mazingira mazuri ya uwekezaji, hivyo anatarajia kuwekeza zaidi kwani mbali na kutaka kupata faida kama mfanyabiashara anataka kuwa sehemu ya kutengeneza ajira zaidi kwa wananchi.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Ikulu imeeleza kuwa Dangote pia amekanusha taarifa kuwa anataka kuagiza makaa ya mawe kutoka nje ya nchi. Amesema anashangazwa na taarifa hizo kwani makaa ya mawe ya Tanzania yana ubora zaidi na ni bei nafuu kuliko makaa ya mawe kutoka nje.

Aidha, amesema kuwa anatarajia kutoa ajira nyingine mpya zaidi ya 1,500 kwa Watanzania na kwamba atanunua kila rasilimali/malighafi za uzalishaji hapa hapa nchini.

“Kazi yetu hapa Tanzania ni kuja kutengeneza ajira na ndio maana tunakataa gypsum au makaa ya mawe [kutoka nje], tutatumia kile kinachozalishwa hapa nchini,” alisema Dangote.

Naye mwenyeji wake, Rais John Magufuli amemhakikishia kuwa Serikali yake itamuwekea mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji.

Rais Magufuli amemtaka mfanyabishara huyo kununua gesi moja kwa moja kutoka TPDC badala ya kununua kutoka kwa watu wa kati wanaonunua kutoka katika shirika hilo la Serikali lenye dhamana ya kusimamia nishati ya Mafuta na Gesi.

“Wapiga dili ndio waliokuwa wameuingilia huu mradi. Sasa hivi wameshindwa na watalegea moja kwa moja. Kwa sababu Dangote wamemuona mwenyewe yuko hapa, na amezungumza nyie wenyewe mmemsikia kwamba hataagiza makaa yam awe au gypsum kutoka nje” alisema Rais Magufuli.

Kona ya Penzi: Jinsi ya kumjibu mpenzi anapouliza ‘Unanipenda Kiasi Gani?’
Messi, Suarez wakalishwa kitako kumwaga wino mpya Barcelona