Mtoto Mariam Ibrahim Mwema (17) ambaye alikuwa akisumbuliwa na tatizo la INTESTINAL OBSTRUCTION amerejea nchini akitokea India alikokuwa kwa muda wa takribani miezi mitatu iliyopita akipata matibabu ya ugonjwa huo.

Mariam alisumbuliwa na tatizo hilo la tumbo tangu akiwa na miaka 7 na kusababisha utumbo wake kupooza na hivyo kutokuweza kula chakula zaidi ya vitu vya majimaji na maumivu ya tumbo yalikuwa ni sehemu kubwa ya maisha yake.

Mariam alitibiwa hapa nchini hadi kufanyiwa upasuaji wa tumbo takribani mara kumi pasipo mafanikio, hivyo Madaktari bingwa wakashauri apelekwe India kwa matibabu zaidi lakini kutokana na hali ya kimaisha ya wazazi wake pamoja na kumpenda sana binti yao, hawakuweza hadi pale Dar24 Media ilipoibua taarifa za mateso ya Mariam, ndipo wadau kadhaa waliona na kuguswa na tatizo la Mariam na kuwezesha kumsafirisha kwenda India Desemba 2017.

Mariam alitibiwa katika hospitali za Apollo na Fortis zilizopo mjini New Delhi, na hatimaye Machi 16, 2018 mtoto Mariam amerejea nchini na kupokelewa kwa furaha na ndugu, marafiki na jamaa zake katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam.

Aidha, kwa mujibu wa madaktari, Mariam mwenyewe pamoja na mama yake aliyemsindikiza nchini India, Mariam anaendelea vizuri na ataendelea kutumia dawa kwa muda wa miezi sita akiwa chini ya uangalizi wa hospitali ili kuendelea kuimarisha afya yake.

Wakizungumza na waandishi wa habari uongozi wa Dar24 kupitia mwakilishi wao Christopher Kika, ameishukuru sana Kampuni ya DataVision International ambao ndiyo washiriki wakuu kwa kushirikiana nao bega kwa bega kuhakikisha mtoto Mariam anapata matibabu na kuwa salama hatimaye atimize ndoto zake za udaktari.

Pia amewashukuru wadau wote walioshiriki kwa hali na mali katika kufanikisha zoezi hili, kama Amifan, ID Cards Solutions, Serena Hotels, MacLeans BeneCIBO, OnDemand na watu mmoja mmoja waliofanikisha kuendesha kampeni ya TUKO PAMOJA kuchangisha fedha na hatimaye Mariam kwenda kutibiwa India.

Aidha, Ametoa shukurani kwa viongozi mbali mbali wa Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa pamoja na Maafisa elimu Kinondoni kwa kutoa baraka zao kuweza kumsaidia mtoto Maria, pia uongozi pamoja na walimu wa shule ya Sekondari Kawe Ukwamani anakosoma Mariam.

“Wapo waliotoa fedha na wengine muda wao kumuombea Mariam; wote tunawashukuru sana. MUNGU awabariki sana kwani Mariam amerejesha tabasamu na matumaini” amesema Kika

Kampeni ya TUKO PAMOJA ni kampeni endelevu inayolenga kuwasaidia watoto wenye umri chini ya miaka 18 wenye matatizo mbali mbali ya kiafya.

Video: Diamond aachia ngoma mpya na msanii toka majuu ''African Beuty''
Mugabe atoa dukuduku baada ya kung'olewa madarakani

Comments

comments