David Adedeji Adeleke maarufu kama Davido, ameweka rekodi ya aina yake wikendi iliyopita baada ya kuujaza uwanja wa O2 wa jijini London nchini Uingereza.

Davido, ‘Mtoto wa Bilionea’ kama anavyopenda kutambulika, aliuza tiketi zote za show yake katika uwanja huo unaobeba takribani watu 20,000.

Kwa tukio hilo, Davido amezigusa rekodi za wasanii wakubwa wa Marekani waliowahi kujaza uwanja huo akiwemo Rihanna, Jay Z, Elton John, Celine Dion, Britney Spears, Kanye West  na Drake.

Hata hivyo, amekuwa msanii wa pili wa Afrika kuishangaza dunia  ya muziki kwa rekodi hiyo baada ya ‘Mnaija’ mwenzake, Wizkid kufurikisha mashabiki kwenye uwanja huo Juni 2018; na kuwa msanii wa kwanza mwenye umri mdogo lakini pia kutoka Afrika kuandika rekodi hiyo.

Katika asali ya shangwe la show hiyo iliyoshereheshwa na muigizaji nguli wa Uingereza, Idris Elba, Davido aliweka tone la kasoro baada ya kuchelewa kuanza show kwa takribani dakika 65.

Hata hivyo, mkali huyo wa Nigeria aliyesindikizwa na mkali wa Dancehall kutoka Jamaica, Popcaan alifanikiwa kuwasahaulisha mashabiki ‘subira’ waliyolazimika kuitumikia, akiwasha moto na nyimbo zake kali zenye mahadhi ya Afrika, akifungua na ‘Aye’.

Davido akisalimiana na Idris Elba, kulia na jinsi show ilivyokuwa

Davido alikuwa msanii wa kwanza wa Afrika kusaini dili na lebo ya kimataifa ya Sony/RCA mwaka 2016, ingawa wengi hawakuiamini habari hiyo, kazi alizoanza kudodosha ziliwafanya wainue mikono, na wikendi iliyopita ameingia kwenye vitabu vya historia ya O2.

BTW : Inabidi ukumbi huo uandaliwe upya…  Diamond, Ali Kiba, Vanessa Mdee wana ‘warmup’…! Inshallah!

 

[youtube https://www.youtube.com/watch?v=-huj_S1x1tY]

 

 

Video:Ndoto za wazazi zapelekea Mariam kuongoza kitaifa
Video: Mnara wa Azimio la Arusha wageuka Chanzo cha ajira