Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wazazi wote nchini waendelee kufuatilia nyendo za watoto ili wasijiingize kwenye mtego wa dawa za kulevya na wala wasisubiri vijana wao waanze kutumia.

Majaliwa amesema hayo leo Juni 29, 2017 kwenye maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani, iliyoadhimishwa mjini Dodoma, ambapo ameeleza kuwa Serikali imeadhimia kupambana vilivyo dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya na kuhakikisha inakuwa historia nchini.

Amesema Serikali imejidhatiti kuhakikisha kuwa uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya unadhibitiwa kikamilifu nchini na katika kutimiza azma hiyo, ambayo pia inaelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Serikali ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Dawa za Kulevya kwa kuanzisha chombo cha kisheria cha kupambana na biashara hiyo, ambayo imeongeza adhabu kwa wanaoshiriki.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha chombo hicho kinachoongoza mapambano ya dawa za kulevya ili kiendelee kufanya kazi kwa weledi na kwa kutumia mbinu za kisayansi.

“Tunaponadi uchumi wa viwanda lazima tuwe na nguvu kazi yenye siha njema kuweza kushiriki kwenye kazi halali za kujenga Taifa letu na yeyote anayetaka kudhohofisha nguvu kazi ya Taifa letu au kuhujumu jitihada za uchumi wa viwanda atashughulikiwa bila huruma,” amesema.

Kufuatia kauli mbiu ya maadhimisho hayo kitaifa ya ‘Tuwasikilize na Kuwashauri Vijana na Watoto ili Kuwaepusha na Dawa za kulevya.’ Majaliwa amesema kauli mbiu hiyo imetokana nan a takwimu za waathirika wakubwa wa dawa za kulevya ambao ni vijana wenye umri kati ya miaka 15-35.

“Hili ndilo kundi kubwa kwenye jamii jetu na ndilo tegemeo kubwa kwa ustawi wa nchi yetu. Hili ndilo kundi litakalotoa askari wa kulinda Nchi yetu, wanasiasa wa kuongoza Taifa letu na wataalamu mbalimbali wa kuisaidia Tanzania,” amesema.

 

Video: Wazee Chadema wapinga vikali kauli ya Mwinyi
Video: CCM waridhishwa na utendaji kazi wa JPM