Hatimaye wale maadui waliogeuka kuwa marafiki, Meek Mill na Drake wamewapa mashabiki kile wanachotaka kwa kuachia video ya wimbo mpya ‘Going Bad’.

Video ya wimbo huo ambao unamilikiwa na Meek Mill iliyoongozwa na The Kid Art, imebeba michezo inayoaminika kuwa ni ya Wamarekani Weusi Watata wanapokuwa na pesa. Michezo ya kugonganisha magari ya kifahari, kutembea kwa tambo za kibabe wakiwa na makundi na mingine.

Mwaka 2015, ulikuwa mwaka mgumu zaidi kwa uhusiano wa wakali hawa wa michano ambapo walitupiana mistari konde kwenye nyimbo zao (diss track) na kutoleana maneno makali ya kejeli na matusi.

Hata hivyo, Novemba mwaka jana mambo yalibadilika baada ya Meek Mill kutoka jela. Drake aliungana na wasanii wengine katika kampeni ya kushinikiza Meek aachiwe huru, hivyo alikuwa sehemu ya waliofanikisha hatua hiyo.

Baada ya kutoka jela, Meek alionesha nia ya kurejesha urafiki uliokuwa umegeuka uhasimu.

“Nafikiri imetuchukua wote kupitia magumu. Ni wakati wa kuonesha upendo sasa. Kwahiyo ilikuwa sahihi kuungana na mtu ambaye niliwahi kufanya naye biashara. Tulichofanya ni halisi na hatukufanya kwa mapenzi ya watu tu,” alisema Meek Mill kwenye mahojiano na Vulture.

Drake alimpandisha Meek Mill jukwaani kwenye ziara yake kwa mara ya kwanza, na waliahidi kutoa wimbo wa pamoja. Ahadi imetimia saa chache zilizopita kwa kuachia ‘Going Bad’.

Mashabiki kupitia YouTube wameanzisha mjadala wa nani amemfunika mwenzake, ingawa wote wanakubaliana kuwa ni ngoma kali.

Angalia hapa:

Lissu akutana tena na kisiki cha Masilingi Marekani, atangaza upasuaji mwingine
LIVE BUNGENI: Yanayojiri Bungeni jijini Dodoma

Comments

comments