Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameupongeza Mradi wa Utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi (TACIP), unaoratibiwa na Kampuni ya DataVision International chini ya usimamizi wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).

Gambo alitoa pongezi hizo wakati alipotembelewa ofisini kwake jijini Arusha na waratibu pamoja na wasimamizi wa mradi huo, wakiongozwa na Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza.

Alisema kuwa mradi huo utafuta kilio cha muda mrefu cha wasanii katika jiji hilo ambao walikuwa wakitamani kufikiwa moja kwa moja na Basata kama hatua ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili. “Kwa muda mrefu wasanii wa jiji la Arusha walikuwa wakiuliza iko wapi Basata tujadili kwa pamoja namna ya kutatua changamoto zetu. Ni jambo zuri kuona Basata imekuja kuwatambua wasanii kupitia mradi huu wa TACIP ambao naamini utaleta suluhisho la matatizo mengi na kilio cha wasanii hawa,” alisema Gambo.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha alisema mradi huo ambao unalenga katika kuwatambua wasanii wa sanaa za ufundi ili kuwawezesha kuwapa thamani na kuuza kwa urahisi bidhaa zao kwenye masoko ya kimataifa, ni fursa ya kuongeza elimu kwa wasanii hususan katika kutumia teknolojia iliyopo kujipatia kipato.

Awali, Katibu Mtendaji wa Basata, Mngereza alisema kuwa mradi huo umelenga katika kuwaongezea thamani wasanii na kuonesha mchango wao katika kuchangia pato la Taifa pamoja na kuongeza fursa ya ajira rasmi.

Mtaalam wa Teknlojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutoka DataVision International, Dkt. Shabani Kiwanga alisema kuwa kampuni hiyo iliamua kutengeneza kanzi data yenye manufaa kwa wasanii katika mlengo wa kuwainua kiuchumi na kutangaza bidhaa dhao katika masoko ya kimataifa, ikiwa ni hatua ya kuungana na juhudi za kulifikisha Taifa katika uchumi wa kati.

Naye Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA), Adrian Nyangamalle alisema kuwa mradi wa TACIP ni mkombozi wa sanaa za ufundi nchini akitoa mfano kuwa asilimia 5.7 ya ajira nchini inaundwa na wasanii. Hivyo, ni muhimu tasnia hiyo kupewa kipaumbele ili kulinda kazi za sanaa na kuongeza thamani ya wasanii.

TACIP ni mradi wa utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi Tanzania ambao umeanzishwa na kampuni ya kizawa ya DataVision International iliyoko jijini Dar es Salaam, inayojishughulisha na masuala ya Teknlolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Tafiti na Mafunzo, ambapo wanatekeleza mradi huo kwa kushirikiana na Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA) chini ya Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo. Mlezi wa mradi huo ni Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Januari 9, 2019
Wenyeviti wagomea kikao kisa diwani kukaimisha nafasi yake kimya kimya

Comments

comments