Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche amesema kuwa anakusudia kumfikisha mahakamani, Mkurugenzi wa Kampuni ya CZI, Cyprian Musiba kwa kumtaja katika orodha ya watu kumi ambao ni hatari kwa usalama wa taifa.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Dar24 Media, ambapo amesema kitendo cha Musiba kumtaja katika orodha hiyo kinahatarisha usalama wake.

Amesema kuwa kitendo hicho kinalengo la kumchafua kisiasa, kumpotezea uaminifu kwa wananchi na wapiga kura wake pia kuhatarisha mfumo mzima wa maisha yake.

Akizungumza na vyombo vya habari siku chache zilizopita jijini Dar es salaam, Cyprian Musiba alitaja orodha ya majina kumi ya watu ambao alidai kuwa ni hatari kwa usalama wa taifa.

“Huyu Musiba amefanya kitendo kibaya sana, na kama kutumika anatumika vibaya sana kwani kuwataja watu na kuwahusisha katika tuhuma nzito kama hizo tena bila ushahidi wowote ni kitu hatari, ninamfungulia mashtaka ili akathibitishe tuhuma hizo mahakamani,”amesema Heche

Hata hivyo, Dar24 Media bado inaendelea kufanya mawasiliano na watu waliotajwa katika orodha hiyo ili kuweza kufanya mahojiano nao.

Magazeti ya ndani na nje ya Tanzania leo Machi 1, 2018
Treni zagongana, 15 wapoteza maisha