Siku chache baada ya kuachia rasmi albam ya ‘DAMN’, rapa Kendrick Lamar amevikuna vichwa vya wadau wa muziki ambao baadhi wamempa taji la kuwa rapa bora kuwahi kutokea, au rapa mkali zaidi aliye hai, jambo lililoibua mjadala mzito.

Wiki iliyopita, DJ Peter Rosenberg wa Hot 97 alisema kuwa baada ya kuachia DAMN, Kendrick Lamar amesakafia taji lake la ufalme na kwamba kwa sasa hakuna rapa duniani mkali kama yeye. Kauli hiyo hata hivyo imekumbana na pingamizi kubwa kwenye mitandao huku Eminem akitajwa zaidi kuwa ndiye mwenye nafasi hiyo.

“Eminem anaweza kurap, Nas pia anaweza kurap na hata Big Pun lakini siamini kama yeyote kati yao anaweza kurap vizuri zaidi kuliko Kendrick Lamar,” alisema DJ Rosenberg.

“Kendrick ndiye rapa bora zaidi aliyewahi kutokea. Hakuna mtu yoyote anayeweza kurap kwenye hii sayari ya dunia kumzidi Kendrick Lamar,” alisisitiza.

DJ huyo alimpima pia Kendrick na Jay Z na kudai kuwa ingawa Jigga ana pesa na mitindo mikali ya kuchana, bado kwenye upande wa michano kwa sasa hakuna anayemgusa Lamar.

Hata hivyo, kauli hiyo iliibua mijadala mikali, lakini tathmini ya kwenye mitandao ya kijamii ilionesha kuwa jina la Eminem ndilo lililopewa nafasi zaidi kukosoa mtazamo huo. Cha kushangaza, majina makubwa kama Jay-Z, Nas, 2Pac na BIG yayakutajwa kwa wingi kama jina la Eminem.

Kendrick alivyoanza kuchafua hewa:

Mwaka 2013, ulikuwa mwaka wa aina yake kwenye muziki wa hip hop, baada ya Kendrick kutema moto kwenye wimbo wa ‘Control’ alioshirikishwa na Big Sean.

Katika shairi lake lilibatizwa jina ‘control verse’, alitamba kuwa yeye ndiye mfalme wa New York, Mfalme wa Pwani zote (East Coast & West Coast) na kwamba anatumia mkono wake mmoja kuzichezesha pwani hizo mbili.

“I’m mackaveli’s offspring I’m the King of New York, King of the Coast, One hand I juggle them both” Lamar alitema cheche kwenye Control.

Kauli hiyo iliwaamsha wengi, akiwemo Eminem ambaye alipofanya mahojiano na BET, alisema kuwa amependa alichokifanya Kendrick kwakuwa kinaongeza chachu kwenye hip hop. Lakini akadai kuwa hakukuwa na jipya kwani tayari wao walishafanya hivyo kabla.

“Ninapenda kitu anachokifanya Kendrick, anaendeleza kitu ambacho hip hop inataka na kuifanya iendelee kuwa ya kuvutia. Alichokifanya kwenye Control Verse ni kizuri, lakini sisi tulishafanya nyimbo za aina hiyo kabla yeye hajafanya hiyo,” alisema Eminem.

50 Cent aliwahi kusema kuwa Eminem ndiye rapa mkali kuliko yoyote aliye hai na kwamba anayetaka kubisha aanzishe mashindano naye au asimame naye halafu aone atakavyofunzwa michano.

Hata hivyo, hakuna bifu kati ya Eminem na Kendrick Lamar. Eminem alimpa shavu Kendrick kwenye ‘Love Game’.

Video: 'Kama unaishi kwa sababu ya filamu lazima upige kelele' - JB
Mradi wa Kinyerezi kuzalisha Megawati 575