Rais John Magufuli, amewasihi wanafamilia wa marehemu Dk. Didas Masaburi aliyewahi kuwa Meya wa jiji la Dar es Salaam, kushikamana kwa upendo bila kubaguana ili wasimpe nafasi shetani kuwavuruga.

Akizungumza leo katika ibada ya kuaga mwili wa Marehemu kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli aliwatambua wanawake watano wa Marehemu na kuondoa ombwe lililokuwepo baada ya kutajwa mwanamke mmoja pekee aliyetambulika.

“Ninafahamu alitajwa mke mmoja wa marehemu. Mimi ninafahamu wake wa marehemu wako wanne… watano hivi,” alisema Rais Magufuli. “Katika tamaduni za kiafrika, kuwa na wanawake wawili, watatu hadi kumi ni jambo la kawaida. Kwahiyo napenda kuwapa pole sana wake wote wa marehemu Dk. Masaburi,” aliongeza.

msiba-wa-masaburi

Aidha, Rais Magufuli alieleza kuwa ingawa imetajwa idadi ya watoto kadhaa lakini watoto waliopo wanaweza kuwa zaidi ya idadi inayotajwa, hivyo aliwataka kwa pamoja kushikamana wakiongozwa na kijana wa kwanza.

“Ninawaomba ninyi watoto mkashikamane. Mkamtangulize Mungu. Baba yenu aliwapenda, mkifarakana mtamletea mateso makubwa, kwa sababu aliwapenda wote na hakuwabagua na ndio maana mahali pa kwenda kuzikwa amechagua mahali pa wote,” alisema Rais Magufuli.

magufuli-masaburi

Dk. Masaburi amezikwa leo katika Chuo cha ugavi na ununuzi cha IPS kilichoko Chanika wilaya ya Ilala, chuo ambacho hadi anafariki dunia alikuwa Mwenyekiti wake wa Bodi.

Ofisi ya chama cha Donald Trump yapigwa bomu la kienyeji
GK aitamani Bifu ya Diamond na Ali Kiba, ’ningeichochea’