Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Ruangwa na mkoa mzima wa Lindi kuchangamkie fursa ya kulima Mihogo na Alizeti kwa sababu mazao hayo yana uhakika wa soko.

Majaliwa ametoa wito huo wakati akizungumza na wananchi katika vijiji mbalimbali vya wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi ambako anapita kuwasalimia wananchi wa jimbo lake akiwa katika mapumziko ya siku nne ya mwisho wa mwaka.

“Nimekuja na fedha, wangapi wanataka kupata fedha?” alihoji Waziri Mkuu katika mikutano yake na kuitikiwa “Sisi” na umati wa watu walionyoosha mikono juu kuonesha kuwa wako tayari kupokea fedha hizo. Mikutano hiyo ilifanyika kwenye vijiji vya Namilema, Mbuyuni, Nandandara, Namkonjera, Muhuru, Chikundi, Chibula na Matumbu.

“Mnataka fedha siyo? Fedha iko shambani! Nimewaletea fursa ya mwekezaji anayetaka kununua mihogo yote katika mkoa huu,” alisema Waziri Mkuu na kusababisha kicheko kwa watu waliokuwa wakinyoosha mikono yao.

Amewataka wananchi hao kulima mtu mmoja mmoja au jiungeni kwenye vikundi ili mpate ekari tatu hadi nne kwa sababu mna uhakika wa soko. Mwekezaji huyu anataka kununua mihogo yote na ya wilaya hii peke yake haitoshi kiasi ambacho anataka. Kwa hiyo tumekubaliana na wabunge wenzangu kwamba kiwanda hiki kitajengwa Nanjilinji ambako ni katikati ya mkoa ili iwe rahisi kusomba na kupeleka mazao hayo,” alisema.

Majaliwa amesema mwekezaji aliyepatikana (bado ni mapema kumtaja) yuko tayari kufuata mazao waliko wakulima na atakuwa akiwalipa hukohuko. “Yeye anachotaka ni mihogo ya kutosha, ndiyo maana nawasisitizia muanze kulima zao hili kwa wingi cha msingi mfuate kanuni bora za kilimo,” aliongeza.

 

Ndege zisizo na rubani kuanza kutoa huduma za kiafya Tanzania
Cheche Akabidhiwa Mikoba Ya Zeben, Kali Ongala Kung’olewa Majimaji FC