Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amepokea ripoti ya uchunguzi wa  ajali ya kivuko cha MV Nyerere kutoka kwa kamati iliyoundwa na Serikali kwa ajili ya kuchunguza ajali hiyo.

Majaliwa amepokea ripoti hiyo leo Oktoba 25, 2018 kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati  hiyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstafu, Jenerali George Waitara, kwenye makazi ya Waziri Mkuu, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuishikuru kamati hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kazi kubwa waliyoifanya ambayo imethibitisha umakini wao.

Pia ameipongeza kamati hiyo kwa namna walivyotumia muda wao vizuri kwa kufanya kazi hiyo na kutoa mapendekezo kwa Serikali juu ya mambo waliyoyabaini.

“Nimepokea taarifa kwa niaba ya Serikali, Serikali itafanya mapitio ya taarifa yote na viambatisho vyake na itapitia kwa kina mapendekezo mliyoyatoa ambayo yote yatafanyiwa kazi.”

MV Nyerere ilipinduka na kuzama Septemba 20, mwaka huu katika ziwa Victoria ambapo Watanzania zaidi 200 walipoteza maisha na wengine Zaidi ya 40 waliokolewa.

Septemba 24 mwaka huu kwenye kijiji cha Bwisya katika kisiwa cha Ukara, wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza, Waziri Mkuu alitangaza kamati ya kuchunguza ajali ya kivuko cha MV Nyerere yenye wajumbe saba ambayo iliyoongozwa na Jenerali mstaafu, Waitara.

Aliwataja wajumbe wengine ni aliyekuwa Mbunge wa Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi, Mhandisi Marcelina Magesa, Wakili Julius Kalolo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Bi. Queen Mlozi, ambapo alisema wajumbe hao wanapaswa kuikamilisha kazi hiyo ndani ya mwezi mmoja.

Putin aeleza anavyosoma hatua za Marekani, ‘piga tukupige’
Kesi ya viongozi wa Chadema yapigwa kalenda