Leo Aprili 21, 2017 mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA) Dkt. Elly Macha aliyefariki Machi, 31, 2017 katika hospitali ya New Cross Wolverhampton nchini Uingereza umeagwa wa wabunge katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma kisha kufirishwa kwenda nyumbani kwake Usa River mkoani Arusha.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameungana na wabunge katika kuuaga mwili wa Dkt. Elly Macha na ametoa pole kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, familia marehemu pamoja na wabunge wote.

Majaliwa amesema enzi ya uhai wake marehemu Dkt. Elly alitoa mchango mkubwa na ushauri mzuri katika masuala ya elimu na uboreshaji wa maeneo ya watu wenye ulemavu.

Awali akisoma wasifu wa marehemu, Mbunge wa Iringa Mjini, Mheshimiwa Mchungaji Peter Msigwa alisema Dkt. Elly alipata ulemavu wa macho akiwa na umri wa miezi mitano baada ya kuugua ugonjwa wa surua.

Mchungaji Msigwa alisema pamoja na kuwa na ulemavu huo wa macho lakini haukuwahi kuwa kikwazo kwake kwani aliweza kufanya jambo lolote lililokuwa ndani ya uwezo wake.

Dkt. Elly alizaliwa Juni 18, 1962 kwenye kijiji cha Kirua Vunjo mkoani Kilimanjaro, ambapo mbali na wadhifa wa ubunge pia  aliwahi kuwa Mshauri Mwelekezi wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu vya Afrika Mashariki.

Aidha, mwili wa Dkt. Elly Macha unatarajiwa kuzikwa kesho nyumbani kwa wazazi wake katika kijiji cha Kirua Vunjo mkoani Kilimanjaro.

Video: Diamond azindua 'Chibu Perfume', atoa neno kwa wasanii nchini
Video: Airtel yazindua duka la huduma kwa wateja Manyara