Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali inapenda kuona maeneo yote nchini yakiwa katika hali ya utulivu  bila ya kuwepo kwa migogoro ya aina yoyote na ikitokea ni vema ikawa inapatiwa ufumbuzi kwa wakati ili shughuli za maendeleo ziweze kufanyika kwa ufasaha.

Amesema hayo katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa Spika, Bungeni mjini Dodoma, ambapo alikuwa anapokea taarifa ya Kamati Shirikishi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ya kushughulikia mgogoro wa matumizi ya ardhi kwenye pori tengefu la Loliondo mkoani Arusha, ambapo atatoa maelekezo baada ya kuisoma.

Majaliwa aliunda kamati hiyo, Desemba mwaka jana, mara baada ya kumaliza ziara ya kikazi mkoani Arusha huku lengo la kamati hiyo ikiwa ni kutaka kupata muafaka wa matumizi ya rasilimali zilizoko katika eneo hilo ili kila upande uweze kutekeleza majukumu yake bila ya kuathiri mwingine na kuwezesha wananchi wote kunufaika na rasilimali zilizoko katika eneo hilo.

“Serikali inataka watu wote tuwe kitu kimoja katika kutunza maeneo yetu, lakini pia shughuli za wananchi nazo ziweze kuendelea ili Watanzania wote tuweze kunufaika na rasilimali zilizoko kwenye maeneo yetu,” amesema Majaliwa.

 

Haji Ugando Kuitema Simba SC
Young Africans, Tanzania Prisons Kumalizia Robo Fainali ASFC